PPC yafanya tathmini mradi wa sauti yangu, amani yangu, hatma yangu.

 

 NA HAJI NASSOR, PEMBA.
MRADI wa miezi sita wa ‘sauti yangu, amani yangu, hatma yangu’ unaotekelezwa na Klabu ya waandishi wa habari wa Pemba PPC, tayari umemaliza robo ya kwanza kwa mafanikio makubwa.

Akizungumza katika mkutano wa tathmini, Mratibu wa mradi huo Ali Mbarouk Omar ,mbele ya wasimamizi wa waandishi wa habari ‘mentors’ na wajumbe wa kamati tendaji ya PPC, alisema kwa robo ya kwanza kila kichopangwa kimefanyika.

Alisema, moja ya kazi hiyo ni uzinduzi wa mradi, mafunzo kwa waandishi wa habari, wadau wa amani, pamoja na mafunzo kwa wasanii wenye maudhui ya ujenzi wa amani.

Alieleza kuwa, mradi huo ambao unakusudia kuweka jukwaa la ulinzi wa amani ndani ya jamii, baada ya mafunzo hayo waandishi wa habari, wameanza kuandika habari za ujenzi wa amani.

Mratibu huyo alifafanua kuwa, waandishi hao wa magezeti, tv, redio, mitandao ya kijamii tayari baadhi yao wameshaanza kuzichapisha na kutangaazwa katika vyombo vyao.

“Leo (jana) tupo kwenye kikao cha robo ya mradi huu, lakini niwambie wajumbe kuwa mafanikio yameanza kufikiwa kwanza kuwa kutekelezwa kile kilichopangwa,’’alieleza.

Katika hatua nyengine Mratibu huyo wa mradi wa sauti yangu, amani yangu hatma yangu kutoka PPC Ali Mbarouk Omar, alisema wamepanga kutengeneza mchezo wenye mwelekeo wa ujenzi wa amani.

Mapema akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa PPC Bakari Mussa Juma, aliwataka wasimamizi hao ‘mentors’ kuharakisha baadhi ya waandishi ambao hawajakamilisha.

Akichangia kwenye mkutano huo, msimamizi wa vipindi vya redio na tv, Khadija Kombo Khamis, alisema wamefikia asilimia 85 ya kuwasimamia waandishi waliowasilisha mawazo yao.

Hata hivyo mjumbe wa kamati tendaji wa PPC Asha Mussa Omar, alipongeza kazi inayoendelea kufanywa na waandishi wa habari.

Mradi wa ‘my voice, my peace, my future’ ambao ni wa miezi sita, unatekelezwa na PPC kwa ushirikiano na tasisi ya Search for Common Ground na the foundation for Civil Society kwa ufadhili wa Umoja wa nchi za Ulaya ‘EU’.