Sunday, November 24

Wajasiriamali Pemba wapewa mbinu kuukimbia umaskini

IMEANDIKWA Na Gaspary Charles- TAMWA-Pemba

WAJASIRIAMALI kisiwani Pemba wametakiwa kuongeza ubunifu wa kazi zao kwaajili ya kujitangaza na kuongeza wigo wa uuzaji wa bidhaa wanazozalisha ili kuendelea kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika mkutano wa kamati ya biashara kwa ajili ya kubadilishana mawazo kwa wajasiriamali ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, mwezeshaji
wa mkutano huo, Hamad Hassan Chande amesema ili bidhaa ya mjasiriamali iweze kupendwa ni lazima iongezewe ubunifu.

Aliongeza kwa kuwataka wajasiriamali hao kuacha kuogopa kukabiliana na changamoto za kibiashara na badala yake watumie changamoto hizo kama silaha ya kubuni njia mpya ya uendelezaji wa shughuli zao.

“Ujasiri na uthubutu kwa mjasiriamali katika kuchukua uamuzi mgumu ya kukabiliana na changamoto katika utekelezaji wa shughuli zake ndiyo sifa kuu na muhimu kwa mjasiriamali hivyo tusiogope kukabiuliana
na changamoto kwani siku zote mjasiriamali anahitaji changamoto zaidi ili kukuza ubunifu wake.”

Katika hatua nyingine mwezeshaji huyo aliwataka wajasiriamali hao kuweka nguvu zaidi katika matumizi ya mitandao ili kuongeza wigo wa soko kupitia mitandao hiyo.

“Tuchangamkie fursa iliyopo kwenye mitandao ya kijamii kwani mitandao ndio sehemu kuu kwa sasa ambayo mtu unaweza kuuza bidhaa zake kwa haraka na kuwafikia wateja wengi zaidi kwa wakati mmoja” alisema.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Fatma Moh’d Juma, alishukuru TAMWA Zanzibar kwa kuwezesha kutolewa kwa mafunzo hayo na kuahidi kuanza kutumia mitandao ya kijamii kutangaza bishara yake ili engo lake la
kujiinua kiuchumi lieweze kufanikiwa kwa urahisi.

“Niwashukuru sana TAMWA Zanzibar kwa nafasi hii ya leo nimejifunza mengi sana kupitia mafunzo haya na sasa nimetoka na wazo la kuanza kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii ili kazi zangu ziwafikie wengi zaidi duniani.” alisema.

Kwa upande wake, Salama Omar Salum, alisema mafunzo hayo yamewawezesha kupata mbinu mpya za kujasiriamali na kuachana na dhana ya kufanya kazo zao kwa mazoea jambo linalopelekea kushindwa kukidhi mahitaji kamili ya soko.

Alisema, “Kupitia mkutano huu tumejifunza umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora hitajika na kuacha kutengeneza bidhaa zetu kwa mazoea kwani kufanya hivyo kumekuwa kukitupunguzia imani ya wateja dhidi ya
biashara zetu.”

Mapema afisa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi TAMWA ofisi ya Pemba, Asha Mussa Omar alisema chama kupitia mradi huo kinaendelea na juhudi za kuhakikisha wanawake Zanzibar wanajikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za ujasiriamali.