Sunday, November 24

Mahakama yamrejesha uraiani aliyedaiwa kumuingilia mlemavu Pujini

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAHAKAMA ya mkoa Chake Chake, imemuachia huru, kijana Abdalla Khatib Abdalla miaka 25 wa Pujini, aliyekuwa akituhumiwa kumuingilia mwanamke mwenye ulemavu wa akili, baada ya mahakama hiyo kubaini utata juu ya eneo alililodaiwa kuingiliwa mwanamke huyo.

Hakimu wa mahakama hiyo Luciano Makoye Nyengo, alisema kuwa, amelazimika kumuachia huru mtuhumiwa kwa vile, shahidi mmoja alidai mwanamke huyo aliingiliwa kichani tena chini ya Muwembe.

Alisema, ilipofika wakati wa shahidi muathirika ambae ana ulemavu wa akili, aliimbia mahakama hiyo kuwa, aliingiliwa na mtuhumiwa ndani ya nyumba eneo la Pujini na sio kichakani.

“Shahidi mmoja alidai kuwa, tukio la kuingiliwa kwa mwanamke huyo lilifanyika kichakani, ingawa alipokuja muathirika wa tukio, aliieleza kuingiliwa ndani ya nyumba na sio kichakani,’’alisema Hakimu.

Hakimu huyo alisema, kuwa kutoka na hitilafu hizo ambazo kwa upande mmoja zimeathiri kesi hiyo, ndio maana mahakama ikamua kumuachia huru mshitakiwa huyo.

Kasoro nyingine ambayo iliishaiwishi mahakama hiyo kumuachia huru mshitakiwa huyo, ni taarifa ya daktari ambae alimfanyia uchunguuzi muathirika Julai 1, mwaka jana wakati tuko hilo lilitokea Juni, 26 mwaka huo huo.

“Hapa pana muda wa wastani wa mwezi mmoja, sasa haingii akili kuwa tukio litokee kisha uchunguuzi wake ufanywe kwa siku kadhaa, hii ni kasoro pia,’’alisema Hakimu huyo.

Pamoja na hakimu kumuachia huru mtuhumiwa huyo, haki ya rufaa imetolewa kwa yeyote, ambae hakuridhika na hukumu hiyo iliyotolewa Augusti 17, mwaka huu.

Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Juma Ali Juma, alidai kuwa shauri hilo lipo kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Baada ya hukumu, Wakili huyo wa serikali alionesha nia ya kukata rufaa, kutokana na kutoridhika na hukumu iliyotolewa mahakamani hapo.

Awali mshtakiwa huyo alidaiwa kuwa, Juni 24 mwaka jana majira ya 1:15 asuhuhi, eneo la Pujini wilaya ya Chake Chake, isivyo halali, alimuingilia kimwili mwanamke mwenye ulemavu wa akili mwenye miaka 18.

Ilidaiwa kuwa, mshtakiwa huyo Abdalla Khatib Abdalla, alifanya tendo hilo huku akijua kuwa, muathirika ni mwenye ulemavu wa akili, ambapo ni kosa kinyume na kifungu cha 116 (1) sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018.

Miezi mitatu iliyopita, mtuhumiwa mwengine Ali Yussuf Mohamed miaka 20 wa Ole wilaya ya Chake Chake, aliekuwa akikabiliwa na tuhuma za kumtorosha na kumbaka mtoto wa miaka 16 mwenye ulemavu wa akili, tokea Novemba mwaka 2017, nae aliachiliwa huru.