Sunday, September 8

Mgombea ubunge Ole kupitia cha UMMA kuving’arisha vikundi vya wanawake akishinda

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo wa Ole kwa tiketi ya chama cha Ukombozi wa UMMA, Maryam Saleh Juma, amesema iwapo atapewa ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo, atahakikisha vikundi vya ushirika vya wanawake anavipatia mitaji, na kuwa kimbilio kwa wengine wanaobeza.

Alisema, bado kundi kubwa la wanawake wanaonekana kutoviunga mkono vikundi vya ushirika, kwa kule kukosa mitaji na mikopo yenye masharti nafuu, ambapo kama akipata ridhaa hilo ndio kipaumbele chake.

Mgombea huyo ubunge ameyaeleza hayo, alipokuwa akizungumza na pembatoday, juu malengo na azma yake ya kuomba nafasi hiyo Jimboni humo.

Alisema, hamu na ari yake ya kuwawezesha wanawake ipo ndani ya moyo wake, na ndani ya mwaka mmoja baada ya kuingia bungeni, wanawake wa Jimbo hilo watakuwa na maisha mazuri kupitia vikundi vya ushirika.

Mgombea huyo alisema, ameshafanya utafiti mdogo na kugundua kuwa, kwa maisha yalivyo sasa, lazima kila mwanamke hata aliyemo ndani ya ndoa awe na mtaji wake wa kujipatia kipato.

“Mimi nawaomba wananchi wa Jimbo la Ole wanikopesha kura zao ikifika Oktoba 28,ili niwalipe maendeleo endelevu ambapo kwa wanawake ni kupitia kwenye vikundi vya ushirika,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo ubunge wa Jimbo la Ole wilaya ya Chake Chake kwa tiketi ya chama cha ‘UMMA’ Maryam Salhe Juma, amwaaahidi wananchi hao kama wakimchamgua, atatenga siku maalum ya kukuata na wanawake na wanaume.

Alifahamisha kuwa, bado Jimbo la Ole, halijapa mbunge anaejali shida za wananchi, kwani wengi wao baada ya kuchaguliwa huyahama majimbo kwa visingizio cha vikao.

“Wanawake na wanaume wanashida zao mbali mbali zinazokwamisha kufikia ndoto zao, sasa wakinichagua kuwa mbunge, nitawatengea siku yao maalum ya kukutana na mimi,’’alifafanua.

Aidha mgombea huyo, alisema kama akipata ridhaa atahakikisha hakuna kijiji ndani ya Jimbo hilo, chenye ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa saa 24.

Kuhusu huduma za afya, alisema atanunua gari maalum kwa ajili ya wagonjwa na mama wajawazito, pale wanapopata uhamisho kutoka vituo vyao vya afya na kwenda hospitali za rufaa.

Mgombea huyo ubunge, alisema vijana wa Jimbo hilo, atawapatia mitaji maalum, kwa ajili ya kuibua biashara ambazo wakizifanya, wataondokana na ulazima wa kuajiriwa serikali.

“Vijana walio wengi hasa wa Jimbo la Ole, wanadhani huwezi kujiwekeza kwenye biashara, kilimo au ufugaji na kusahau ajira ya serikali, sasa kama wanikichagua hilo litawezekana,’’alieleza.

Khamis Mohamed Makame wa Ole, alisema kwa mwaka huu ataachana na kumpigia kura mbunge mteule wa chama chake cha ‘ACT-Wazalendo na atampa kura mgombea huyo.

Alisema, Jimbo hilo halijawahi kujitokeza mgombea mwanamke ambapo kwa mwaka huu, ameanza kuwashahiwishi wenzake kuona wanamuunga mkono mgombea huyo.

Fatma Haji Makame na Asha Abeid Omar walisema wamevutiwa mno na sera ya kuwawezesha wanawake kupitia mbunge huyo, ndio maana wameanza kuwashahiwishi wenzao.

Muume wa mgombea huyo ambae aligombea udiwani kupitia chama cha ACT, Hamad Khamis Mwalimu, alisema hadi sasa hajaamua rasmi kumuunga mkono mgombea huyo (mke wake) na kwanza, anafuatilia sera zake.

“Hii ni demokrasia, yeye ameamua kugombea chama cha ‘UMMA’ na amepitishwa, na mimi sikubahatika kupitia ACT-Wazalendo, sasa nafuatilia mikutano yake na kusikiliza ahadi,’’alieleza.

Baadhi ya wanachama wa CCM, CHADEMA na ACT-Wazalendo waliokataa majina yao yasichapishwe, wamesema kura ni siri yao, na hadi sasa hawajakuwa na uamuzi wa mgombea yupi wampe.

Awali Mratibu wa TAMWA Pemba, wakati akizungumza kwenye mikutano ya kuwahamasishwa wanawake kuingia majimboni, aliwataka wapiga kura kuona wanawapa kura za ndio wagombea wanawake.

Uchaguzi mkuu wa vyama vingi nchini, nunatarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu kwa kumchagua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani.