Friday, December 27

DK. Shein : CCM haikukosea kumteua dk: Hussein Ali Mwinyi kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar.

NA HAJI NASSOR, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Mhe: dk: Ali Mohamed Shein, amesema CCM haikukosea kumteua dk: Hussein Ali Mwinyi kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar, kwani anasifa ya uchapakazi uliotukuka, ambao wagombea wa vyama vyengine hawana.

Dk: Shein, ameeleza hayo uwanja wa Gombani kongwe wilaya ya Chake Chake Pemba, alipokuwa akizungumza na mamia ya wanaCCM na wananchi wengine, kwenye uzinduzi wa kampeni kwa chama hicho, na kumnadi mgombea huyo wa urais wa Zanzibar.

Alisema, CCM daima imekuwa ikiteua wagombea wake wa nafasi mbali mbali wenye sifa bora za kufanya kazi kwa nidhamu, uhodari na usiopendelea mtu wala kundi lolote, na kuwaomba wananchi kumchagua kwa kishindo mgombea huyo.

Alieleza kuwa, mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM dk: Hussein Ali Mwinyi, amekuwa akifanya kazi kwa uhodari, tokea alipokuwa katika nafasi mbali mbali za serikali na hivyo akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar kwenye uchaguzi ujao.

“Mpeni kura za ushindi dk: Hussein Ali Mwinyi maana ni mtu bora na mchapakazi hodari na katika mazingira yoyote anafaa, maana amekuwa akipanda siku hadi siku, kwenye kuwatumikia wananchi,’’alisema.

Aidha Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe: dk Ali Mohamed Shein, amewaomba wanaccm na wale wa vyama vyengine, kuhakikisha wanampigia kura za ndio mgombea huyo, ili apate ushindi ambao utaviziba mdomo vyama vyengine.

Alieleza kuwa, daima CCM imekuwa ikivuna ushindi tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini na uchaguzi wa mwanzo wa mwaka 1995, ambapo na mwaka huu 2020 kwa aina ya mgombea aliyesimamishwa kunatarajiwa ushindi mnono.

“Mpeni kura dk: Mwinyi, ili ushindi wake usiwape la kusema washindani wake na kwa jinsi ilani yetu ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 ilivyo nzuri, ushindi hauna wasi wasi,’’ alifafanua.

Katika hatua nyingine rais huyo wa Zanzibar, alisema kutokana na CCM kutekeleza yale wanayoaahidi kwa wananchi kimeendelea kuwa chama bora, na imara ukilinganisha na vyama vyengine.

“Kila mmoja amekuwa akikiunga mkono chama cha Mapinduzi, kutokana na kutekeleza yale wanayoahidi mbele ya wananchi, na leo tunajivunia, ubora na uimara huo,’’alisema.

Mapema mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Mhe: dk: Hussein Ali Mwinyi, alitaja maeneo 10 kwa ufupi ambayo anatarajia kuanza nayo mara akipata ridhaa ya wananchi.

Alisema, suala la udhalilishaji linaendelea kumuumiza kichwa, hivyo akiingia madarakani, tatizo hilo atalipa kipaumbele, ili kuona kundi la wanawake na watoto linaishi kwenye mazingira bora na imara.

“Kila ninapopita wananchi wa Zanzibar wanalilia suala la udhalilishaji kuwa limekuwa kubwa mno, sasa hili lazima nilifanya miongoni mwa vipaumbe vyangu,’’alieleza.

Jengine alilowaahidi wananchi wa Zanzibar kulitekeleza kwa haraka, ni kukuza uchumi samba na kuongeza pato la taifa kutoka thamani ya shilingi trilioni 2.4 mwaka 2015 hadi kufikia thamani ya shilingi trilioni 3.1 mwaka 2019.

Kuhusu kuongeza makusanyo ya ndani, kutoka shilingi bilioni 428.511 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 748.9 mwaka 2019 pamoja na kupunguza utegemezi wa bajeti na kufikia asilimia 5.7 na kuvuuka lengo linaloanishwa na kufikia asilimia 7.

Aidha mgombea huyo wa urais wa Zanzibar aliwaahidi wananchi hao, kama akipata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar atajenga barabara kwa kiwango cha lami, zenye urefu wa kilomita 198 kwa Unguja na Pemba.

“Tunaposema tunaimarisha uchumi, lazima tuangalie pia na ujenzi wa barabara, ndio ambao utarahisuisha kila kitu,’’alieleza.

Kuhusu sekta ya utalii, alisema atahakikisha anatekeleza mpango shirikishi wa uendelezaji utalii (ISAP) na mradi wa big Zed ili kuongeza thamani ya utalii wa Zanzibar na kupanua wigo wa ubora wa na upekee wa bidhaa zinatolewa kwa wageni.

“Tukifanya hivi tutaongeza idadi ya watalii kutoka 338, 264 mwaka 2019 na kufikia 850,000 mwaka 2020/2025 na kuengeza siku za ukaazi kutoka wastani wa siku saba, kwa mwaka 2019 hadi kufikia siku nane kwa mwaka 2025”,alifafanua.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Sadala ‘Mabodi’ alisema CCM itendelea kuwatumikia wananci bila ya ubaguzi wowote.

Awali rais huyo wa Zanzibar aliwanadai wagombea uwakilishi na ubunge wa majimbo yote ya Pemba, na kisha kuomba kura kwa wananchi.