Saturday, December 28

Maalim Seif kukuza pato la mwani akiingia Ikulu tu

MGOMBEA  wa urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha ACT- Wazalendo maalim Seif Sharif Hamad, amesema endapo wananchi wa Zanzibar watamchaguwa na kumuweka madarakani,  atahakikisha wakulima wa mwani wanapata faida kwa kuweka bei nzuri ambayo itakidhi machungu ya kilimo hicho.

Maalim Seif aliyaeleza hayo huko Tumbe wilaya ya Micheweni Pemba, wakati akizungumza na wakulima wa mwani pamoja na wavuvi wa eneo hilo, katika ziara yake kisiwani humo.

Alieleza kuwa, wanunuzi wa mwani  wanakuwa wanawadhulumu  wakulima kwa kununua zao hilo kwa bei ya chini ya shilingi 600 kwa kilo moja.

“Tukingia madarakani nitahakikisha Serikali yangu inawahudumia wakulima wa mwani, kwa kuwapatia vyombo ambavyo vitafika maji makubwa, ili waweze kulima mwani bora wa Cotonee ambao unabei kubwa katika soko la dunia,” alieeza.

Mapema wakulima wa zao hilo walimuambia Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kuwa, wakulima na wavuvi wengi wanafariki baharini kutokana na  vyombo vidogo vidogo, wanavyotumia na kukosekana vyombo vya uokozi.

Halima Ali ambaye ni mkulima, alisema wamekuwa wakipoteza nguvu kazi kutokana kulima mwani kwenye maji makubwa kwa kutumia vyombo vidogo.

“Licha ya kwenda mbali na kina kikubwa cha maji,  bei hii haituridhishi hata kidogo nyonga zote zimekufa kwa kuinama siku nzima halafu eti bei ya mwani kilo moja shilingi 60,” alieleza.

Kufuatia kilio hicho Maalim Seif alisema mara tu akiingia madarakani, atahakikisha wavuvi watakopeshwa boti za bei nafuu ili waweze kuvua katika maji makubwa na kuwa salama.

“Tutahakikisha KMKM wanajeshi wa maji wanakuwa na boti nzuri na zenye mwendo mkubwa zikipata tetesi za ajali kwa wavuvi wafike haraka kwa ajili ya uokozi,” alifahamisha maalim Seif.

Alisema atahakikish wavuvi wote wanakuwa na mawasiliano na wanamaji hao,  ili likitokea tatizo waweze kufanya mawasiliano ya haraka.

Alieleza kuwa katika Serikali yake atahakikisha bei ya mwani inafikia tsh 1000 kwa kilo na kuwapatia vifaa vyote ambavyo vitarahisisha katika kazi zao.

Maalim Seif anaendelea na ziara yake kisiwani Pemba kwa kukutana na makundi mbali mbali, ili kuwaeleza azma yake pindi akiingia madarakani.