Saturday, December 28

DK. Shein aweka jiwe la msingi Pemba.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampunzi ya Zanzibar Construction Company Limited Kepteni Hamad Bakari Hamad, kuhusu eneo litakalojengwa Viwanda mbali mbali huko Chamanange II, kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi Kiwanda cha kusafiria Mwani.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amesema kuwa sula la viwanda kwa Zanzibar ni suala la miaka mingi sana, kabla ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 na baada ya Mapinduzi, ikiwemo viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa.

Alisema viwanda hivyo vilikuwa vya sabuni, usumba, mafuta ya nazi, viwanda vya soda, maziwa, Mapinduzi ya mwaka 1964 ndio yaliobadili maendeleo hayo.

Dk.Shein aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba, mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kusarifia Mwani uliokwenda sambamba na Uzinduzi wa eneo la Viwanda Chamanangwe II Mkoa wa Kaskazini Pemba.

“Zanzibar ilikuwa imenawiri kwa viwanda vidogo vidogo, ikiwemo viwanda vya maziwa, mterekta, soda, kiwanda cha Rangi kilikuwa ndio pekee kwa Afrika Mashariki”alisema.

Serikali ya awamu ya 7 ya Mapinduzi ya Zanzibar huwezi kuzungumzia suala la ajira bila ya kuwa na viwanda, lazima kuwepo na watu wa kuwekeza ndio ikatengenezwa sera ya viwanda ili Zanzibar kuwa ya viwanda vya uhakika.

Akizungumzia kuhusu zao la Mwani, Dk Shein alisema biashara ya mwani Zanzibar ilikuwa ikifanywa na serikali, hivyo ZSTC imeanza upya kununua mwani kutokana na wakulima baada ya kuona wanyonywa na wanunuaji wa zao hilo.

Aliwataka wananchi kutokushangaa kuwa zao hilo kufikia kilo shilingi 3000, kwani mwani utahitajika zaidi kwa kusarifiwa vitu mbali mbali ikiwemo faluda na soko lake tayari lipo.

“Sisi tunajiandaa kuutunza na kuuthamini mwani, kama ilivyo zao la karafuu, mwani ni zao letu la baharini, soko sio tatizo tatizo ni kuulima kwa wingi na akinamama wameshafundishwa kulima mwani huo”alisema Dk Shein.

Aliwataka akinamama kuendelea kulima mwani ili kujiwekeza sawa pale kiwanda kitakapoanza kazi na kunua mwani huo, kwani Serikali ya awamu ya Saba na Nane imdhamiria kuwainua akinamama katika kuhimili uchumi wa kisasa wa buluu.

Alisema kuanzishwa kwa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 55, litakalokuwa na viwanda mbali mbali litakuwa ni mkombozi mkubwa kwa vijana kupata ajira, kwani baada ya kiwanda cha mwani ni kiwanda cha Chumvi kinachofuata.

Alisema ujenzi wakiwanda hicho utagharimu shilingi Bilioni 7.5 ambazo ni fedha kutoka mashirika ya serikali, ikiwemo ZSTC, Bima, ZSSF, PBZ na Bandari, kiwanda hicho kikiwa na lengo la kusarifu bidhaa mbali mbali za mwani.

“Chamanangwe II hii ya viwanda itakuwa maarufu dunia, mazao mbali mbali yatatoka hapa na kwenda kuuzwa nje ya nchi, baada ya kusarifiwa hapa, jiwe la msingi la mwani tumeweka leo na hili eneo zuri”alisema.

Kwa upande wake waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Balozi Amina Salim Ali, alisema eneo hilo la viwanda kwa pemba ni la kwanza katika kuelekea uchumi wa viwanda, kwani mradi huo utakapokamilika utaweza kubadilisha eneo hilo kwa Zanzibar kutokana na fursa nyingi za kazi, uzalishaji.

Alisema eneo la Chamanagwe II litakuwa ni kituo kikubwa kwa Zanzibar cha kusindika mazao ya matunda mboga na viungo ambavyo vinasoko kubwa sana katika nchi za SADEC na Asia, Ghuba, ulaya na marekani, kutokana na bidhaa zitakazosindikwa katika eneo hilo.

Alifahamisha kuwa serikali inaendelea kuandaa sera ya kuelekea uchumi wa bulu, ambapo wazo hilo tayari imeshaanzwa kutekelezwa kwa kuwekwa jiwe la msingi kiwanda cha mwani.

Alisema mwanzo bei ya mwani ilikuwa ni shilingi 600 na sasa bei ni shilingi 1800 kwa kilo ya mwani, huku shirika la ZSTC likiwa ndio wanunuzi wakubwa wa zao hilo.

Naye katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar Juma Hassan Reli, alsiema uwepo wa eneo hilo utaweza kufungua milango ambapo kutakuwa kunasarifu bidhaa mbali mbali zitakazokuwa zinauzwa katika masoko ya utalii na kuzuwia fedha nyingi ambazo mahoteli yalikuwayakitumia kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Alisema serikali kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali imeweza kulipa fidia kwa wananchi wa eneo hilo shilingi Milioni 332 kwa shehia ya Mchanga mdogo, Kambini na Kiuyu Minungini, huku Milioni 251 kutolewa kwenye mashamba na Milioni 81 zimetolewa kwa fidia kwa wenye maboma.