MGOMBE Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha wananchi CUF, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba amesema kuwa CUF inaomba kura kwa sababu chama hicho katika vyama vyote ndicho kinachosimamia haki sawa kwa wananchi wote.
Alisema katika jambo ambalo CUF walifanikiwa kulipata Zanzibar katika mapambano ya kisiasa, ni katiba inayozungumzia uwepo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa.
Profesa aliyaeleza hayo wakati wa ufunguzi wa Kampeni za chama hicho, zilizofanyika katika uwanja wa michezo Tibirinzi mjini Chake Chake Pemba, huku zikihudhuriwa na wanachama na wananchi wa chama hicho.
Alisema CUF imekuwa ni waasisi wamaridhiano, waasisi wa mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ambayo imepelekea kuwepo kwa serikali ya umoja wa Kitaifa.
“Ndugu zangu nyote mnakumbuka tuliingia katika mgogoro wa chama na Maalim ndio chanzo cha yote baada ya kutaka Lowasa kuwa Rais baada ya mgombea kutoka Chama chake”alisema.
Aidha aliwataka wananchi kuwa makini na kauli za Maalim Seif, kwani sio mkweli kwa kuwataka wananchi kuwa tayari jambo lolote lile, huku akiwataka wananchi wa Pemba kutokuwa tayari kusikiliza kauli za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa.
Alivitaka vyombo vya Dola na Tume za Uchaguzi kuwa CUF inahitaji haki, kwani CUF inaamini haki sawa kwa wote na kuahidi kushiriki katika uchaguzi, aliyeshinda ndio anayepaswa kutangazwa.
Lipumba aliwasisitiza wanachama na wananchi wasikubali kupoteza kura zao, kwani wakiipigia ACT maalim Seif hawezi kuwa Rais wa Zanzibar, sambamba na kuvitaka vyombo vya dola na serikali kutokuchokozeka na wanasiasa, kwani wananchi wanataka uchaguzi wa amani na CUF inataka uchaguzi wa amani.
“Msingi wa amani ni haki, tume ya uchaguzi inahitaji haki, musikubali wenzangu kuingizwa katika machafuko, watu wanaochochoa machafuko haipendei mema Zanzibar na kutaka kujijengea umaarufu kisiasa”alisema.
Hata hivyo aliwataka wasikubali kubaguliwa, wazanzibari na watanzania bara wote ni wamoja, hivyo wananchi wanapaswa kuwa wamoja na walinda amani.
Kwa upande wake mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF Mussa Haji Kombo, alisema kuwa iwapo wananchi wakimchagua kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha anaondosha ubaguzi katika masuala ya elimu, kwa kuhakikisha Pemba inakuwa na vyuo vikuu kama ilivyo Unguja.
Aidha aliwaomba wananchi kuachana na ubaguzi na badala yake kuwa wamoja kwa lengo la kuigomboa Zanzibar, huku akiwatakwananchi kuhakikisha wanamuamini na kuwa kiongozi wao.
Naye katibu Mkuu wa CUF Haroub Mohamed Shamsi, aliwataka wananchi kukichagua chama cha CUF, ili kuongoza serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Mmoja ya viongozi wa Chama hicho Kutoka Tanzania Bara Yassin J. Mrotwa, alisema CUF Tanzania bara iko pamoja na wananchi wa Zanzibar huku akiwataka Oktoba 28 kuhakikisha wanakichagua chama hicho ili kiweze kuongoza nchi.
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Chake Chake Abdalla Seif Omar, aliwataka aliwataka vijana na wananchi kulaani vikali kauli znazotolewa na baadhi ya wanasiasa za kuhatarisha uvunjifu wa amani ya nchi, pamoja na kuwanasihi vijana kutokushiriki katika vitendo vyovyote viovu, kwani vijana CUF bado inawahitaji.
Mkutano huo pia ulipata nafasi ya kuwatambulisha wagombea Ubunge, Udiwani na Uwakilishi wa chama hicho kwa mikoa miwili ya Pemba.