WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed, amewataka wananchi wa Zanzibar kutokukubali kuchokozeka badala yake kuendelea kudumisha amani ya nchi.
Alisema dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwaelimisha wananchi, juu ya suala zima la kufahamu umuhimu wa amani katika nchi kabla na baada ya uchaguzi.
Waziri Aboud aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Kisiwani Pemba, juu ya kuwahamasisha wananchi utunzaji wa amani ya nchi kuelekea uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 2020.
Alisema ni wakati muhimu sasa kwa wanasiasa kukubali kufanya uchaguzi mkuu kwa salama na amani, pamoja na kuwa walinzi wan chi katika kipindi hiki.
“Sisi ni walinzi wa nchi yetu, kumeanza kutokeza dalili ambazo sio nzuri, wananchi serikali imejipanga kuhakikisha inafanya uchaguzi wake kwa amani”alisema.
Aidha alifahamisha kuwa haipendezi kuona au kutokea kwa mwananchi yoyote, anatokea kushiriki au kuharibu au kufanya vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani nchini, kwani vyombo vya sheria viko macho.
“Hatupendi kuona kuna vitisho au kutia hofu wananchi kwa aina yoyote vile, wananchi wanahitaji amani na kuendelea na shuhuli zao za ujenzi wa taifa”alisema.
Aidha aliwataka wananchi wa Kisiwa cha Pemba, kuendelea kufuata sheria za nchi na watakao vunja sheria hizo, hatua kali watachukuliwa, kwani Zanzibar haipendi kuona watu wanafanya mambo ambayo yanahatarisha amani.
Katika siku za hivi karibuni, viongozi mbali mbali wakiwemo wanasiasa wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamisisha wananchi, kuendelea kutunza amani ya nchi na kutambua kuwa baada ya uchaguzi kunamaisha.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba hivi karibuni aliwataka vijana kuhakikisha, hawanunuliwi na wanasiasa pamoja na kuwa mstari wambele katika uvunjifu wa amani, badalayake wanakuwa walindaji wakubwa wa amani hiyo.