Saturday, December 28

Wapigwa mapanga msikitini.

 

NA MWANDISHI WETU.

 

 

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Mohamed Aboud Mohamed, amesema katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu sio vizuri mtu kuchukua sheria mikononi mwake jambo ambalo linaweza kupelekea uvunjivu wa amani ndani ya nchi.

Aliyasema hayo katika Hospitali ya Vitongoji mara baada ya kuwatembelea na kuwafariji majeruhi ambao walipigwa mapanga alfajiri ya kuamkia jana huko Kangagani Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema, mtu yoyote haruhusiwi kuchukua sheria mikononi mwake kwani Serikali na vyombo vya usalama vipo macho na vinaendelea kufanya ulinzi katika maeneo yote ya nchi.

Alieleza, kwa sasa msako mkali utaendelea kufanyika na kwa yoyote ambae atashiriki kwa njia moja ama nyengine kuharibu amani na utulivu uliopo huku hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Na kwa wale wanasiasa ambao wana maneno ya jazba na kusababisha wengine kuvunja amani wachunge sana kauli zao kwani unapotoa kauli za kuashiria uvunjifu wa amani yanayotokea ni kama haya”, alisema.

Alieleza, wanasiasa ni vyema kushindana kutokana na sera zao na sio maneno ambayo yataleta taharuki na migogoro kwani amani inapoharibika watu wote watakua ni waathirika wa janga hilo.

Waziri huyo alifahamisha kuwa, Serikali haipo tayari kuona amani inavunjwa hivyo kwa msingi huo itachukua hatua kuwatafuta wale ambao wamehusika na kuwatia mbaroni huku mkondo wa sheria ukichukua nafasi yake.

Daktari dhamana wa hospitali ya Vitongoji Sharif Hamad Khatib alisema, mnamo wa majira ya saa 12:00 asubuhi wamewapokea majeruhi watatu kutoka kijiji cha Kangagani ambao baada ya uchunguzi wa madaktari walibainika kwamba wameshambuliwa kwa kitu chenye ncha kali.

Aliwataja, majeruhi hao ni Khamis Nyange Makazi Prof Gogo (65) ambae alipata jeraha kubwa katika sehemu ya shingo, Bakar Ali Hassan (55) ambae ni mwenyekiti wa maskani ya CCM Kangagani alipata jeraha katika mkono wa kulia na Kombo Hamad Yussuf (73) ambae ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Wete alipata jeraha katika bega la kulia.

Alifahamisha kuwa, wagonjwa hao kwa sasa wanaendelea vyema na madaktari wanaendelea na kuwafanyia uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wanapona vizuri.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis  alisema, Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na hakuna mtu ambae amekamatwa hadi sasa .

“ Nikweli tukio hili limetokea katika kijiji cha Kangagani na tunaendelea na uchunguzi ingawaje hadi sasa hatujamkamata mtu yoyote kuhusiana na tukio hili,”alisema

Kwa upande wake  Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Ahmed Khamis Makarani, ambako majeruhi wamelazwa alisema kweli tukio limetokea Mkoa wa Kaskazini lakini majeruhi wapo katika Hospitali ndani ya Mkoa wake hivyo atashirikiana na wenzake kujua namna gani watakamilisha ukamataji wa wahalifu hao.

Kamanda Makarani aliwataka wananchi kujitahidi kutii sheria bila shuruti kwani alisema mtu anapofanya uhalifu wa aina yoyote jeshi la polisi litahakikisha linamtia mkononi.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Wete Pemba, Kamanda Mohammed Mussa Mkobani, aliwataka wananchi wa Wilaya hiyo kuwa na amani huku Serikali ikishirikiana na vyombo vya sheria ili kuhakikisha muhusika wa tukio hilo anachukuliwa hatua.

“ Tunawataka Wananchi wa Wilaya ya Wete na wengine kuweni na amani kwani vyombo vya Sheria vinawahakikishia usalama wenu na tutahakikisha muhusika anachukuliwa hatuwa,”alieleza.

Kwa upande wake Imamu wa msikiti huo ambae pia ni sheha wa Shehia ya Kangagani  Fakih Omar Yussuf pamoja na waumini wengine waliokuwepo Msikitini hapo wamesema Kijana huyo alifika akiwa ameshikilia panga mkononi na ndilo alilolitumia kuwajeruhi watu hao.

Hata hivyo  majerushi hao walisema, majira ya alfajiri wakiwa msikitini walivamiwa na mtu ambae aliwashambulia kwa mapanga na kumtambua kuwa ni Hassan Abdalla Hassan ambae ni Katibu wa ACT Wazalendo Tawi la Kangagani.