CHAMA cha Alliance For Democratic Change (ADC), kimelaani vikali kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa, ambazo zinaashiria uvunjifu wa amani nchini, huku wakivitaka vyombo vya ulinzi na usalama na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania Jaji Mutungi kutokuvifumbia macho na kuvipuuza.
Chama hicho kimesema kauli hizo za chokochoko hata mwaka 2001, zilikuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi wa siasa wakati wa kampeni, jambo ambalo mwisho wake zilipelekea vurugu na kusababisha taifa kuingia doa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ADC Taifa, Omar Costantino Pweza wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari, huko katika ofisi ya Kanda ya ADC Wawi, kufuatia kujitokeza kwa viashiria vya uvunjifu wa amani Kisiwani Pemba.
Mkurugenzi huyo alisema ADC inalaani vikali kauli hizo zinazopelekea kuashiria uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Taifa.
“Hata sisi baadhi ya vyama tushangaa Kuona ukiukwaji mkubwa katika majukwa kwa dhahiri, ukimya wa jaji Mutungu na ofisi yake ya msajili inatuletea mashaka, kwa sababu kuna kamati ya maadili ya Taifa imeweka wazi kiongozi atakae fanya uchochozi, chama chake kichukuliwe hatua lakini cha kusikitisha mpaka sasa hakuna kitu”alifahamisha.
Alisema ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa kuna vitu wanavilea, hivyo alisema kila taasisi husika inapaswa kuchukua wajibu wake, ili kuifanya nchi iendelea kuwa salama.
Hata hivyo alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukuwa nafasi yake, kwani ADC haiku tayari kuona wananchi wanafanya vurgu kwa sababu ya siasa, kwani wanahitaji wananchi kuishi kwa amani.
“Wapo viongozi katika majukwaa baada ya kuhubiri kuomba kura wanahubiri shari, fitna, chuki jambo hilo halipendezi na kwenda kinyume na maagizo ya mwenyezi Mungu,”alisema.
Aliwataka vijana kujitambua na kuheshimu amani, umoja na mshikamano wao uliopo, hayo mambo wasipoyakemewa viongozi wa siasa kuwa nasauti kubwa, ili kuepusha nchi katika hali ambayo sio sahihi.
Mkurugenzi huyo wa ADC aliwataka viongozi wa vyama vya siasa, kufanya kampeni na kuomba kura kwa amani, kwani Tanzania inahitaji amani na utulivu, wasikubali kutumiwa kuharibu amani ya nchi.
Alisema viongozi wanapaswa kuwafikiria na kuwaonea huruma vikongwe, watoto wadogo, akina mama wajawazito na wagonjwa, kwani ndio waathirika wakubwa panapotokea vurugu.
“Wananchi wanahitaji amani, maisha ya watanzania na wazanzibari ni bora kuliko chochote, kwani hakuna hakuna kiongozi aliye au chama kilicho muhimu zaidi ya amani”alisema.
Aliwasihi wazanzibar kuangalia vyama vinavyowaomba kura, kwani kuna baadhi ya vyama havipendi kuona wananchi wanaishi kwa amani na utulivu, huku akiwataka kuwa kitu kimoja kama walivyofanya wakati wa ugonjwa wa Corona na kuushinda ugonjwa huo.
Hata hivyo alisema aani si sehemu ya serikali, sio sehemu ya vyama vya siasa bali amani ni yawatanzania wote, hivyo wananchi wanahitaji amani iyendelea kuwepo na kulindwa kwa nguvu zote.