Saturday, December 28

Dk. Hussein Ali Mwinyi: kama nikipata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar, nitahakikisha kunatungwa sheria, ambayo itawawezesha wajane kupata haki zao stahili.

NA MWANDISHI WETU, PEMBA .

 

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kama akipata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar, atahakikisha kunatungwa sheria, ambayo itawawezesha wajane kupata haki zao stahili, kama yalivyo makundi mengine.

Alisema anaelewa changamoto kadhaa zinazowakumba wanawake hao, iwe kwa wale wanaoachwa au kufiwa na waume, kwa kukoseshwa haki zao na kutupiwa mzigo wa malezi na huduma kwa watoto.

Mgombea huyo wa urais, aliyasema hayo ukumbi wa zamani wa baraza la Wawakilishi mjini Wete Pemba, alipokuza akizungumza na wanachama wa jumuiya ya wajane Zanzibar kwa upande wa Pemba.

Alisema, anatambua kuwa Zanzibar lipo kundi kubwa la wajane ambalo linaendelea kuteseka na kuhangaika huku na kule na wale wanaume waliowaacha, wakishindwa kuwapata huduma.

Alisema, kwa vile wameshaanzisha umoja wao, kwake itakuwa rahisi kulisaidia kundi hilo ni pale atakapopata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar.

Alieleza, yapo maeneo matatu makubwa ambayo wajane hao wanapaswa kusaidia, ambapo moja wapo ni kupata haki zao kisheria kwa haraka.

“Nikiingia madarakani tu, nitangalia uwezekano mkubwa, ili wajane wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria, maana haiwezekani kuachwa kwako au kufiwa na muume, iwe ndio waishi kwenye mazingira magumu,’’alieleza.

Eneo jengine alililotaja mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kuwa atalishughulikia kama akipewa ridhaa, ni kuwawezesha kiuchumi kupitia jumuia yao.

“Tukiwawezesha kiuchumi wajane wa Zanzibar, itasaidia sana kwa wale ambao pia wana watoto kupata mtaji wa kuwahudumia, ili waishi kwa amani,’’alifafanua.

Hata hivyo alisema hayo yote yanawezekana, ikiwa pia watakiunga mkono chama cha Mapinduzi, kuelekea uchaguzi mkuu wa vyama ving mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika hatua nyingine Dk. Mwinyi amekubali ombi la Jumuiya hiyo kuwa, kama akipata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar, mke wake Maryam Mwinyi awe mlezi wa Jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya wajane Zanzibar Tabia Makame, alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji.

“Tumekuwa kama vile hatuna thamani mbele ya jamii, kwa sababu ya ujane wetu, sasa mgombea urais, tunaomba kama ukitapata ridhaa, utunyamazishe kilio chetu,’’alieleza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Jumuiya hiyo, Mgeni Hassan Juma, alisema wajane wa Zanzibar wamejenga matumaini makubwa na Dk. Mwinyi.

Mapema akizungumza na waalimu wa madrassa na masheikh wa wilaya y Wete, kweye ukumbi wa Jamhuri mjini Wete, Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar, aliwataka viongozi hao kuhubiri amani na utulivu.

Alisema, ibada haitofanyika vyema ikiwa nchi imechafuka kiamani, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuona anaitunza kwa njia ya kuihubiri kila wakati.

Akijibu baadhi ya maswali ya viongozi hao, ambao walitaka kujua, akiwa rais wa Zanzibar atalishughulikiaje tatizo la masheikh wa Zanzibra walioko rumande, ambapo alisema tayari kesi hiyo sasa imeshafikishwa mahakamani.

“Hili la masheikh walioko rumande, tusilijadili sana maana kwanza limeshafikishwa mahakamani, na sasa masheikh hao wanatafutiwa wakili, lakini kesi ikiwa mahakamni haipaswi kuzungumzwa kwanza,’’alifafanua.

Hata hivyo Dk. Mwinyi amewahakikisha waalimu na masheikha hao kuwa, kama akipata ridhaa ya kuwa rais, ataandaa mpango maalum, ili kuimarisha usomeshaji wa kur-ani.

“Ni kweli kwa sasa mfumo ulivyo, watoto wetu wanaelekea mno kwenye elimu ya skuli na muda mdogo ndio unawakuta madrassa hilo sio sahihi, lazima tuandae mifumo ambayo itawapa watoto fursa ya kusoma maeneo yote,’’alieleza.

Aidha mgombea huyo, alisema anakusudia kuona anaziimarisha madrassa za kur-an, kuwapatia vitendea kazi waalimu, mishahara ili wafanye kazi kwa kujiamiani.

“Haiwezekani, waalimu wetu wanaotusomesha elimu itakayotufaa akhera wawe duni, na wengine waendelee kupokea mishahara, lazima na wao tuwawekee utaratibu wa kunufaika,’’alifafanua.

Hata hivyo, aliwaahidi viongozi hao wa dini kuwa akipata ridhaa atarejesh mfumo wa zamani wa kuwapeleke masomoni viongozi wa dini, katika nchi mbali mbali.

“Nakiri kuwa utaratibu wa masheikh na vijana wetu kuwapelekea nje ya nchi kwenda kuongeza elimu ni mzuri, na mimi hili litalifanya,’’alisema.

Mmoja kati ya masheikh hao, Sheikh Mohamed Ismail, alisema kinachowakereketa ni kuona masheikh wenzao hawafikishwi mahakamani na wanaendelea kushikiliwa rumande huko Tanzania bara kwa muda mrefu.

Nae sheikh Mohamed Fumu, alisema kutokana na dhamira yake njema mgombea huyo wa nafasi ya urais wa tiketi ya CCM, watamuunga mkono kwa kumpa kura Oktoba 28, mwaka huu.

“Kwa hakika nyota njema huonekana mapema, maana hili la kukutana na sisi, sio jambo dogo, katika umri wangu huu ni mara ya kwanza, kuitwa na mgombea,’’alieleza.

Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika ziara yake ya kukutana na makundi mbali, alianza na wakulima wa zao la karafuu, viungo, chumvi, wajane, viongozi wa madhebu ya dini, wavuvi na mafundi wa gereji.