RAIYE MKUBWA – WVUSM.
WAFANYAKAZI wa Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Pemba, wametakiwa kuendelea kulinda nidhamu na heshima ya kazi kwa kutozungumzia siasa wakiwa sehemu ya kazi, pamoja na kuacha kujiingiza katika makundi ambayo mwisho wake yatapelekea kuingia matatizoni wakati huu wa kuelekea Uchaguzi.
Hayo yameelezwa na Afisa Mdhamini Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Fatma Hamad Rajab, alipokua akizungumza na Wafanyakazi wa Wizara hiyo katika Ukumbi wa Mkutano wa Wizara ya Fedha na Mipango Gombani Wilaya ya Chake Chake.
Alisema baada ya uchaguzi serikali inaendelea, aliwataka kuendelea kulinda heshima nidhamu ya kazi panoja na kutokujiingiza katika mambo yasiowahusu.
Aidha, amewasisitiza wafanyakazi hao kutokubali kutumiwa vibaya, kuepuka vigenge baada ya kuondoka kazini mambo ambayo yanaweza kuwachafulia maisha yao, huku akiwataka kuwa wazalendo na nchi yao kwa kudumisha amani na upendo.
“Kipindi hiki sio kipindi kizuri hata kidogo, hujuwi yupi aduwi wako au mwema wako, vizuri tukitoka kazini vyombo vya serikali kulazwa katika ofisi za serikali au hata sehemu za Polisi kwa ajili ya usalama”alisema.
Afisa utumishi Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Pemba Mohammed Kombo Juma, amewasisitiza wafanyakazi kuwa wawajibikaji katika majukumu yao na kufuata taratibu zote za uingiaji na utokaji kazini.
Pia amewahimiza kuwa na utaratibu wa kuenda katika Ofisi za ZSSF, kuangalia Michango yao ambayo wamechangia kama imefika au ikiwa kunatatizo waweze kurekebishiwa.
Kwa Upande wake Mratibu Idara ya Mipango Sera na Utafiti Khamis Siasa amewaomba wafanyakazi wenzake kufuata maelekezo ya viongozi wao hasa kipindi hichi cha uchaguzi, kuwataka kutokuthubutu wala kushiriki kufanya vitendo vibaya vitakavyopelekea uvunjifu wa amani.
Nae Muhasibu wa Wizara hiyo Harith Badawi Hamadi, amewashauri wafanyakazi kujenga tabia ya kuenda bank kuchukua taarifa zao za kifedha na kuenda ZSSF kuangalia michango yao kila baada ya muda mfupi.