Thursday, January 16

Mtoto wa miezi saba arudi kwa mama yake.

 

NA MARYAM  SALUM, PEMBA.

 

MTOTO  wa miezi saba aliyekosa  kunyonya maziwa ya mama yake  kwa muda wa wiki mbili, mahakama  ya Mkoa Chake  chini ya hakimu Luciano  Makoye  Nyengo, imefanikiwa kumrejesha mtoto  huyo kwa mama yake,  ili aweze kupata haki yake hiyo.

Mahakama iliesema kuwa chanzo cha mtoto huyo kukosa haki yake hiyo, ni baada ya baba mzazi wa mtoto huyo kuamua kumchukuwa kwa muda wa wiki mbili na kwenda kuishi nae kwenye  familia yake.

Mahakama  hiyo  ilisema kuwa ilipokea ombi hilo kutoka kwa mama mzazi wa mtoto huyo, Zulfa Hassan Ussi mwenye miaka 21, mkaazi wa Machomane, na kudai  mahakama hapo kuwa mtoto wake wa miezi saba  amechukuliwa na mumewake na kuishi nae katika  sehemu nyengine.

“Muheshimiwa nimekuja  katika  mahakama yako kuleta ombi langu  mtoto wangu  wa miezi  saba amechukuliwa  na baba yake mzazi  na  kwenda  kuishi naye  kwenye  familia yake”, alidai.

Alidai kuwa mahakama ndio  itamsaidia  kupewa mtoto wangu, aweze kubaki na mimi kupata haki yake ya kunyonya, kwani huko aliko hapati kunyonya, anateseka  yeye na mimi kwani maziwa  yangu  yamevimba  na kuniuma.

Alidai kuwa mumewake alimchukuwa mtoto  na kuishi nae bila kupata kunyonya  kwa siku kadhaa, jambo ambalo linamfanya mtoto wake  kukosa  haki yake na pia kumuhatarishia maisha yake.

Baada ya ombi la upande wa malalamikaji, hakimu  huyo alikubali ombi hilo,  na ndipo alipomtaka malalamikiwa amabye ni baba mzazi  Said  Seif  Abdalla, akabidhi mahakama mtoto huyo na mahakama iweze kumkabidhi mama mzazi mtoto wake.

Hakimu huyo alisema  kuwa ombi  la muombaji likiwa limewasilishwa  kwa hati ya dharura, mahakama baada ya kupokea ombi hilo,  pande zote ziliweza kupatikana na kusikilizwa.

Katika kusikilizwa kwa ombi hilo, muombaji ambaye ni mama mzazi wa mtoto , pamoja na sababu zilizomo ndani ya hati ya kiapo,  aliiambia  mahakama  kuwa baba mzazi alimchukuwa mtoto kwa lengo baya.

Hata hivyo  kwa upande wa muombewa  ambaye ni baba mzazi wa mtoto,  aliiambia mahakama kuwa ni  kweli mtoto anaumri wa miezi saba,  na kumchukua  kwake  kumesababishwa na mama mzazi mwenyewe.

“Tokea kumchukuwa mwanagu  Arshad  Said  Seif,  ni wiki mbili sasa kutoka  kwa mama yake,  ambaye  ni mke wangu, na sababu zilizonifanya nimchukue mtoto akiwa bado na umri mdogo, mama mzazi anazijua”, alidai.

Shauri hilo limeahirishwa mahaamani hapo, na kupangiwa   tarehe nyengine, ambapo hakimu huyo ametaka lirudi tena mahakamani hapo  novemba 2, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.