Wednesday, January 15

Abdulla Mzee Mkoani Pemba yakabidhiwa Mashine ya kupimia Damu kwa uchunguzi wa maradhi mbali mbali.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Dr. Juma Mbwana { Mambi} akitoa ufafanuzi wa Wizara ya Afya jinsi ilivyojipanga kuhakikisha huduma mbali mbali za Uchunguzi wa Afya zinapatikana katika Hiospitali ya Rifaa ya Abdulla Mzee.

Picha na – OMPR – ZNZ.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema upatikanaji wa Vifaa vya Kisasa vya Afya katika Hospitali mbali mbali Nchini ni mwanzo mwema wa Zanzibar kukomboka katika utoaji wa huduma bora za Afya kwa Wananchi wake.

Alisema mfumo uliokuwa ukitumika wa baadhi ya Wagonjwa kuwasafirisha Tanzania Bara na wengine nje ya Nchi mbali ya kutumia gharama kubwa za Fedha lakini pia ulikuwa ukihatarisha afya za wale wagonjwa wanaosafirishwa wakati tayari wanasumbuliwa na Maradhi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiukabidhi Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba Mashine ya kupimia Damu kwa uchunguzi wa maradhi ya Moyo, Figo, Maini pamoja na vitakasa mikono vilivyotolewa na Mfanyabiashara Maarufu Nchini Nd. Said Nasser Nassor Bopar.

Alisema Serikali Kuu itajitahidi katika kuona vifaa Tiba vinapatikana Nchini ili kwenda sambamba na Sera ya Afya inayoelekeza kwamba huduma za Afya zinawafikia Wananchi wote tena kwa wakati mahali popote pale Mijini na Vijijini Unguja na Pemba.

Akimpongeza Mfanyabiashara Said Bopar kwa Uzalendo wake anaoendelea kuufanya wa kuunga mkono Sekta za Elimu na Afya Nchini Balozi Seif  alisema ni vyema Vifaa vinavyotolewa kwa ajili ya Huduma za Wananchi vikaangaliwa vyema ili vimudu kutoa huduma kwa kipindi kirefu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Watendaji wa Afya hasa Madaktari kuzingatia wajibu wao wa kusimamia Sera ya Matibabu bure iliyoasisiwa na Chama cha Afro Shiray Party mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

 

Alisema haipendezi kuona baadhi ya Watendaji hao wanatumia lugha ya ulaghai kuwafanyia Wagonjwa ambao wana Haki ya kupatiwa Matibabu bure kama ilivyoainishwa kwenye Sera ya Afya na miongozo mbali mbali inayotolewa na Serikali katika Kuona Sekta hiyo muhimu kwa Maisha ya Wananchi inakidhi haja.

Balozi Seif aliutanabahisha Uongozi wa Wizara ya Afya kwamba katika kuona  huduma za Afya zinaimarika vyema na kuwafikia Wananchi, haki za Madaktari ikiwemo posho zao kutokana na  kufanyakazi katika muda wa ziara zinapatikana kwa wakati.

Alisema tatizo kama hilo ambalo pia limekuwa likiripotiwa kwa Watendaji wa Hospitali ya Wete lazima liondoke au kupungua kabisa kwa nia ya kutowavunja moyo Madaktari hao walioamua kujitolea kufanya kazi katika muda wao wote wa saa 24.

“ Mcheza kwao hutunzwa. Hivyo tatizo hili lilokuwa kilio cha muda mrefu lazima lipungue au kuondoka kabisa kwani inashangaza huchukuwa karibu Miezi sita jambo lisilopendeza kabisa”. Alisisitiza Balozi Seif.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Watendaji wa Hospitali ya Abdullah Mzee Mkoani Daktari Mkuu wa Hospitali hiyo Dr. Haji Mwita Haji alisema kupatikana kwa mashine hiyo ni ukombozi mkubwa kwa Wananchi wanaofika kupata huduma za Afya kutokana na maradhi mbali mbali yanayowasumbua.

Dr. Mwita alisema Wananchi wanaofika Hospitali hiyo kufanyiwa uchunguzi wa Damu kutokana na Maradhi mbali mbali wakati mwengine hulazimika kusafirishwa kwenda Unguja au Tanzania Bara mazingira ambayo Familia za Wagonjwa hao hulazimika kutumia gharama kubwa wakati kipato chenyewe hakikidhi.

Daktari Mkuu huyo wa Hospitali ya Abdullah Mzee kupitia Balozi Seif  ameikumbusha Serikali pamoja na Uongozi wa Wizara ya Afya kuongeza uharaka wa ukamilishaji wa baadhi ya Vifaa vilivyofungwa na vinavyotaka kufungwa ambavyo huchelewa kutokana na ubaha wa Fedha.

Mapema kwa upande wake Mfanyabiashara Said Nasser Nassor {Bopar} alisema mfumo wake wa kuunga mkono Sekta za Elimu na Afya Nchini ni dhima anayolazimika kuitekeleza katika kutoa huduma kwa Jamii iliyomzunguuka.

Nd. Bopar alisema huu ni wajibu anaolazimika kuufanya kila Mwanaadamu aliyoruzukiwa neema na Mwenyezi Muungu. Hivyo aliwataka Watendaji wa Sekta ya Afya kuhakikisha kwamba Mashine na Vifaa wanavyokabidhiwa kwa ajili ya kuwasaidia Wananchi wanavitunza ili vidumu kwa muda mrefu zaidi.

Hafla hiyo fupi ya kukabidhi Mashine ya uchunguzi wa Damu pamoja na Vitakasa Mikono ilishuhudiwa pia na Timu ya 30 ya Madaktari Bingwa kutoka Jamuhuri ya Watu wa China ikiongozwa na Dr. Zhuo.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

14/10/2020.