Thursday, January 16

Kuweka mazingira safi ni njia ya kujikinga na maradhi yakiwemo ya mripuko. Waziri Hamad.

 

Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Hamad Rashid Mohammed amewataka wananchi kuongeza juhudi katika kuweka mazingira yao safi na salama ili kuepuka kushambuliwa na maradhi yatakayopelekea kuzorotesha afya zao na kurudi nyuma kimaendeleo.

Muheshimiwa Hamad ametoa wito huo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi katika maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani huko katika Ukumbi wa  Samail Gombani Kisiwani Pemba.

Mh. Hamad amesema ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana ni lazima wananchi wawe katika hali ya usafi wa mazingira yao huku wakidumisha amani iliyopo ili kila mmoja aweze kupata nafasi ya kufanya kazi kwa ufanisi.

“siku zote uchafu ndio ambao unasababisha maradhi na watu wengi huugua kutokana na uchafu” alisema Mh. Hamad.

Amesema mara nyingi kunapotokea maradhi ya Mripuko kama vile kuharisha na kipindupindu jambo kuu linalosababisha maradhi hayo ni uchafu.

Aidha Mh. Hamad amesema  hata ulipotokea mripuko wa maradhi ya corona nchini basi jamii ilihimizwa zaidi kuweka katika hali ya Usafi hasa kuosha mikono kwani mikono ndio chanzo kikuu cha maradhi.

Kwa Upande wake Mkurugenzi kinga Elimu ya Afya Fadhil Mohammed Abdalla amesema kuna maradhi makubwa ambayo mengine ni ya kudumu yatokanayo na  jamii kutokufanya usafi wa kutosha hasa mikono ambayo ni miongoni mwa kiungo  kinachoweza kuchukua wadudu wa maradhi kwa haraka.

“unaweza kugusa sehemu ambayo imekaa wadudu (bacteria) kwa haraka lakini watu hushindwa  kugundua  hivyo hujikuta wanapata maradhi bila ya kufahamu chanzo chake “alisema.

Naye Mkuu wa Elimu ya Afya Halima Ali Khamis amesema Wizara ya Afya ina matumaini makubwa kwamba jamii itaendelea na tabia ya kuosha mikono mara kwa mara kwa maji mtiririko  na sabuni ili kuepuka maradhi ya mripuko yatokanayo na mikono kutokuwa safi.

Mwakilishi kutoka shirika la Afya duniani WHO  Dr. Vendelin Tarmo Simon amesema jamii lazima iwe na uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa kuosha mikono kwani kuosha mikono unaweza unaweza kujiokoa na maradhi  lakini mikono hio hio inaweza  kuhatarisha afya yako wewe na wengine ndani ya jamii.

“kwa kutumia mikono yako unaweza ukachukua wadudu na ukaeneza sehemu nyengine bila ya kujua  na iwapo watu hawana utamaduni wa kunawa mikono  unawekupelekea kunatokea mripuko wa maradhi  bila ya kutarajia.”alisema.

Hivyo amewataka wanajamii kuona umuhimu wa  Ujumbe wa mwaka huu Kitaifa unasema  osha  mikono  Okoa maisha kwani una maana kubwa katika ustawi wa maisha ya baadae.