RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein, amewataka wananchi na watumiaji wa brabara ya Ole- Kengeja,
kufanya kila njia ili kuhakikisha wanaitunza kwa nguvu zao zote,
barabara hiyo ili idumu kwa muda mrefu.
Dk. Shein ameeleza hayo uwanja wa mpira Kengeja wilaya ya Mkoani
Pemba, alipokuwa akizungumza na wananchi wa mikoa mwili ya Pemba, mara
baada ya kuzindua barabara hiyo mpya yenye urefu wa kilomita 35.
Alisema barabara ndio kichecheo kikubwa cha maendeleo ya wananchi kwa
kule kuitumia kwa shughuli zao mbali mbali iwe ni usafirishaji mazao,
hivyo suala la kuitunza ni jambo la lazima.
Alisema, ujenzi wa barabara hiyo umetumia fedha nyingi, hivyo hakuna
budi kuona upo umuhimuwa na ulazima wa kuitunza kwa wananchi, ili
itumike na kizazi kijacho.
‘’Waswahili wanasema kitunze kidumu na kitunze chako mpaka usahau cha
mwanzako, sasa hili linawahusu watumiaji wote wa barabara hii ya
iliyoanzia Ole kupitia Vitongoji, Pujini, Kiwani, Naguji hadi
Kengeja,’’alieleza.
Dk. Shein amesisitiza kuwa barabara hiyo, itakuwa na manufaa makubwa
kwa wananchi wote wa Pemba, kwa kule kuitumia kusafirishia mazao yao
na shughuli nyengine.
Alisema, barabara hiyo sio ya watu maaluma, bali kila mmoja anawajibu
na haki ya kuitumia ili atimize ndoto za maisha yake, kwa vile imekuwa
ni kichecheo kikubwa, cha maendeleo.
Hata hivyo alisema, sasa wananchi wanaweza kuimarisha maisha na uchumi
wao, kwa vile ule usumbufu waliokuwa wakiupata kwa usafiri wa nchi
kavu, sasa umeshaondoka.
“Tumetumia fedha nyingi kuijenga barabara hii, kwa lengo la kuwasaidia
wanachi wetu, ili wapate urahisi wa kuendeleza shughuli zao mbali
mbali,’’alieleza.
Katika hatua nyingine rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mainduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alisema ujenzi wa barabara hiyo,
ulianzia na wazo tokea la rais wa Zanzibar wa kwanza wa Zanzibar,
marehemu Abeid Amani Karume.
Alisema, wazo hilo sasa limetimia baada ya kujengwa kwa barabara hiyo
kwa kutumia wataalamu wa ndani, chini ya Wakala wa Barabara ‘UUB’.
Kuhusu, alama za vijijini ameitka wizara husike kuweka alama za
utambulisho wa vijiji, ili watu waelewe wapi walipo na kuwapa uwelewa
hasa kwa wageni.
Alieleza kuwa, ni vyema kuwepo kwa mabango maalum yanayofahamisha
majina ya vijiji, pamoja na alama za mipindo, daraja kubwa, daraja na
ndogo pamoja na usawa, ili kuwapa ukumbusho watumiaji.
‘’Hili la kuweka alama lifanywe haraka sana, maana barabara imeshaanza
kutumiwa na wananchi kadhaa, sasa ili kuwaepushia na ajali zisizo za
lazima kwa wananchi na madereva wetu,’’alifafanua.
Hata hivyo aliitaka Mamlaka ya Barabara Zanzibar UUB, kufanya
matengenezo ya baadhi ya maeneo ya barabara hiyo, ili kuwakinga
wananchi waliokaribu na barabara hiyo na maji ya mvua hapo baadae.
‘’Wapo wananchi wanajenga karibu na barabara hii ya Ole- Kengeja, sasa
lazima muende kabla hawajamaliza ujenzi, ili isiwe kero hapo
baadae,’’alisema Dk. Shein.
Mapema Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe, wakati akitoa maelezo ya ujenzi wa
barabara hiyo, alisema inaupana wa mita 7.5.
Alisema kukamilika kwa barabra hiyo, sasa Unguja na Pemba kuna
kilomita 1,251.7 za barabara zenye kiwango cha lami wakati Pemba
pekee, sasa ina kilomita 322.8 za zenye kifusi zenye urefu wa kilomita
250.
Alisema barabara hiyo ambayo imepitiwa na shehia 10 ikiwemo ya Ole,
Uwandani, Vitongoji, Pujini, Kiwani na Kengeja, imekuwa mkombozi
mkubwa kwa mtandao wa mawasiliano ya barabara kisiwani Pemba.
‘’Kukamilika kwa barabara hii, sasa kumekuwa na mtandao mzuri wa
mawasiliano ya nchi kavu kisiwani Pemba, jambo ambalo ni utekelezaji
mzuri wa Ilani ya CCM,’alisema.
Aidha Katibu mkuu huyo alisema, awali ujenzi wa barabara hiyo
ulitarajiwa kuanza mwaka 2013, lakini kutokana na changamoto kadhaa
ikiwemo ucheleweshaji wa fedha na vifaa ndio ukaanza mwaka 2016.
‘’Kukamilika kwa barabara hii, sasa ni nafasi kwa wizara yetu
kuielekea barabara ya Kipapo-Mgelema hadi Wambaa ili wananchi wa
maeneo hayo, nao kuwaondoshea usumbufu,’’alisema.
Waziri wa wizara hiyo Sira Ubwa Mwamboya, alimpongeza rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kwa juhudi
zake za kuisimamia vyema Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Alisema, kilichobakia kwa wananchi ni kuona wanaitunza barabara hiyo,
ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutumiwa na wananchi wengine.
Wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, waliipongeza
serikali ya awamu ya saba, kwa kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa
barabara hiyo.
Fatma Hassan Hija na Zainabu Hasnuu Haji walisema barabara hiyo sasa
imemaliza kiu yao ya uasafiri waliyokuwa nayo kwa muda mrefu.
Walisema, sasa wataendesha shughuli zao kwa ufanisi, iwe kusafirishia
mzao,kwenye mjini Chake chake au harakati zao nyingine mbali mbali za
kimaisha.
Bara bara ya Ole- Kengeja yenye urefu wa kilomita 35 ambayo ilianza
ujenzi wake mwaka 2016, ambapo ilihusisha nyumba 452 zilizolazimika
kuvunjwa kupisha ujenzi huo, na shilingi bilioni 4.363 zilitumika kwa
ulipaji wa fidia.
Aidha barabara hiyo yenye daraja 16 makubwa na ndogo ndogo 108,
imegharamiwa na shirika la usafirishaji mafuta duniani ‘OPEC’ kwa
mkopo wa thamani ya shilingi bilioni 30.953, huku serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibra ikichangia shilingi bilioni 2.371 kwa ajili ya
kumalizia ujenzi huo.