Saturday, October 19

DK. Shein azindua BOHARI ya dawa Pemba.

NAIBU Waziri wa Afya Zanzibar Harous Said Suleiman (katikati), akikunjuwa kitambaa kuashiria ufunguzi wa bohari kuu ya Dawa Kisiwani Pemba, kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shien, hafla iliyofanyika Vitongoji Chake Chake Pemba.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amesema kujengwa kwa bohari ya kuhifadhia dawa kisiwani Pemba, litaondosha tatizo la uagiziaji dawa Unguja na kwamba Hospitali na vituo vya afya vyote Pemba vitachukuwa dawa katika bohari hiyo kwa wakati muwafaka.

Alisema hayo ni mafanikio makubwa ambayo hayajawahi kufikiwa, hivyo wananchi na watendaji wanapaswa kulitunza na kulithamini, ili bohari hiyo inadumu kwa muda mrefu na kukidhi mahitaji wa dawa.

Rais Dk.Shein aliyaeleza hayo mara baada ya kuzindua rasmi bohari ya kuhifadhia Dawa, huko Vitongoji Changuo Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kuisni Pemba.

Aidha Dk Shein aliahidi kufanya kila linalowezekana, kuona dawa muhimu zinapatikana katika haospitali na vituo vyote vya afya, kwamba serikali imekuwa na jitihada kubwa ya kuongeza bajeti ya dawa kila mwaka.

“Kwa mfano bajeti imeongeza kutoka bilioni 7 mwaka 2017/2018 hadi kufikia bilioni 17.7 mwaka 2020/2021, pia ameweza kuimarisha huduma za kinga na tiba kutokana na mikakati yake ya kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya kila mwaka,”alisema.

Aakizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Naibu waziri wa Wizara ya Afya zanzibar Harous Said Suleiman, alifahamisha kuwa serikali imeweza kuimarisha huduma mbali mbali zikiwemo za mama na mtoto, kujenga vituo vya afya vipya Unguja na Pemba, huku akiwataka wananchi kutambua maendeleo yanayoletwa na serikali hayachaguwi mtu wala chama.

Alisema Serikali imeelekeza dawa zote zinunuliwe kutoka viwandani na kampuni kubwa kubwa, ni vyema uongozi wa wizara kuweka utambulisho au mihuri maalumu kwenye dawa zinazonunuliwa na serikali, kufanya hivyo serikali na wananchi wataweza kuzitafautisha dawa zinazonunuliw ana serikali na zinazoingia nchini na watu wengine.

“Nadhani kampuni zinazotengeneza dawa hizo, hazitokata kuweka alama maalumu, tunawea kuweka mihuri kwenye vifungashio kwa dawa zinazotolewa kwenye maghala yetu, ili tutaweza kuwabaini wajiriwa wenye tama ya kuuza dawa za serikali”alisema.

Alifahamisha kwamba sera ya serikali ni kutoa matibabu bure, inakuwaje kuona mfanyakazi wa serikali anachukua dawa dawa na kwenda kuuza wa watu binafsi.

Aliwahimiza viongozi na wafanyakazi kufuata miongozi ya wataalamu wa afya, inayohitajika na kuhakikisha bohari zinakuwa safi muda wote, ili kuzihifadhi dawa zisiharibika.

Aliwataka wananchi kujiepusha na tabia ya kutumia dawa bila ya kufuata ushauri kutoka kwa daktari, kwani inaweza kusababisha maradhi mengine kuliko ambayo uliokwenda kutafuta dawa, kwani kuna baadhi ya watu wanashindwa kwenda hospital na badala yake wanatumia dawa tu.

 

Katika hatua nyengine Dk.Shein, aliwasihi wauzaji wa dawa wanapaswa kujiepusha kutoa dawa kwa wingi kwa maslahi ya biashara yake, ili kujali maisha ya mwananchi anayemuuzia dawa hizo, huku akiwataka kutumia vituo vya afya na hospitali za serikali.

Akizunguzmia ujenzi wa bohari ya dawa Vitongozi, alisema ujenzi huop umegharimu jumla ya shilingi Bilioni 2.8, ambapo shilingi Bilioni 2.3 sawa na asilimia 80% kutoka serikalini na shilingi milioni 500 sawa na asilimia 20 kutoka kwa global Faund.

Aidha aliushukuru mfuko huo, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye ujenzi wa bohari kuu ya dawa Pemba,ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoiweka kipindi akifungua bohari ya dawa maruhubi.

Alisema bohari ya dawa la Pemba ni kubwa kuliko la unguja, kwani linaweza kuhifadhi parent 590 za kuhifadhia dawa wakati la unguja linahifadhi parent 550.

Alisema serikali imeweza kuongeza dawa zote muhimu, zinazowatibu wananchi wa Zanzibar zinapatikana katika hospitali za unguja na Pemba, kwa lengo la kuimarisha huduma za afya Pemba, serikali imeijenga upya hospital ya Abdalla Mzee Mkoani na kuipandisha daraja pamoja na hospitali ya Vitongoji, Micheweni, Kivunge Makunduchi na kuzifanya hospitali za wilaya, serikali pia inamkakati wa kuijenga upya hospitali ya Wete ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Naye naibu katibu mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Haliman Maulid Salim, alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya saba, imeweza kudhihirisha utoaji huduma bora kwa wananchi bila ya malipo, kwa ujenzi wa bohari ya dawa Vitongoji ni utekelezaji wa ilani ya CCM, sera ya afya na mikakati ya wizara katika kuimarisha huduma za afya.

Alisema uwepo wa bohari hiyo itaweza kupunguza tatizo la dawa katika vituo vya afya Pemba, la kufuata huduma hiyo katika bohari ya unguja.

Alifahamisha kuwa Wizara ya afya inathamini sana juhudi za serikali katika kuongeza bajeti ya dawa muhimiu na vifaa tiba katika kipindi cha miaka mine mfululizo kutoka bilioni 7 mwaka 2017/18 hadi Bilioni 12 mwaka 2018/19 na kuongezeka tena hadi kufikia bilioni 15 mwaka 2019/20202.

Pia bajeti hiyo imeongezeka tena na kufikia Bilioni 17.7, kutokana nan a ongezeko hilo la bajeti hivi sasa wananchi wanapata dawa za matibabu ya maradhi yenye gharama kubwa kama vile Canser, Diaylsis, Neurosurgery, maradhi ya mifupa na ajali.

“maradhi haya yoite yanahitaji fedha nyingi kwa ununuzi wa dawa zake, pamoja na vifaa tiba na vifaa mbali mbali vya kisasa vya uchunguzi wa maradhi vimenunuliwa vikiwemo MRI,CT-Scan na Dialysis Mchines”alisema.

Alisema miongoni mwa faida zinazopatikana juu ya uwepo wa bohari hiyo, hospitali zitaweza kupata dawa za kutosha kwani bohari hiyo inauwezo wa kuhifadhi dawa zote muhimu na zitakuwa zinapatikana muda wote zitakapohitajika”alisema.

Mapema mkurugenzi Bohari kuu ya dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad, akitoa maelezo ya bohari hiyo kwa mgeni Rasmi wakati akitembelea baada ya kuifungua, alisema uwepo wa bohari hiyo itaongeza upatikanaji wa dawa muhimu za binaadamu kwa wakati.

Alisema pia itaweza kupunguza gharama za usafirishaji wa dawa kutoka unguja, kwa vile bohari litahifadhi dawa nyingi za matumizi kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili.