Wednesday, January 15

Mti mrefu kumbe upo Tanzania.

 

Mti mrefu barani Afrika uko Tanzania, ni kivutio watalii

Mti mrefu zaidi Afrika kivutio kipya cha watalii Tanzania

Mkoa wa Kilimanjaro uliopo kaskazini mwa Tanzania, ni maarufu kwa shughuli za utalii.

Kila mwaka watalii huja kwa lengo la kupanda Mlima Kilimanjaro. Lakini hivi sasa, watalii wamepata kivutio chengine mkoani humo.

Hii ni baada ya serikali ya Tanzania kutangaza kuwepo kwa mti mrefu zaidi barani Afrika. Mti huu aina ya Mkukusu una urefu wa mita 81.5 na unaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).

Ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Dk. Andreas Hemps na mkewe wote kutoka nchini Ujerumani ndio waliobaini kuwepo kwa mti huo umbali wa mita 1600 kutoka usawa wa bahari baada ya utafiti uliohusisha nchi nyengine barani Afrika kwa kipindi cha miaka mitano.

“Nilifika hapa mara ya kwanza siku ya Krismasi mwaka 1996 na nilikuwa meingia kufanya utafiti wa msitu. Niliona miti hii na kusema hii ni kitu kikubwa lakini nilikuwa sijajua kama ni mita 80. Natumia skana ya leza. Napima mara tatu halafu ndio napata urefu kamili. Wageni wengi watafika hapo kushuhudia mti huu, pamoja na watafiti vilevile. Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro pia nayo imeanza kuangalia mazingira haya ili yasiharibiwe,” Dk. Andreas Hemps amemweleza mwandishi wa BBC Aboubakar Famau.

Licha ya mti huu kuwa kivutio ambacho kinaweza kuiingizia serikali fedha za kigeni, lakini changamoto iliopo ni ugumu wa kuufikia mti huo.

Ili kufika katika eneo la Mrusungu ambapo ndipo ulipo mti huo mrefu zaidi, ni safari ya kutembea kwa mguu kwa takriban muda wa saa nne kwenda na kurudi kwa kupita katika milima, mabonde, mito na makorongo.

Kazi iliyofanywa na watafiti hao, inaonekana kuupa heshima mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa jumla na mti huo utaongeza chachu ya watalii kupanda Mlima Kilimanjaro na wengine kwenda kushuhudia mti huo.

 

 

Maelezo ya picha,

Charles Ngendo ambaye ni mhifadhi wa utalii katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro

Kwa upande wake, Charles Ngendo ambae ni mhifadhi wa utalii katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro amesema hifadhi inatarajia kuboresha miundombinu ya kufika katika mti huo ili kuwawezesha watalii kwenda kwani miundombinu ya sasa hivi sio rafiki kwa utalii.

“Niseme tu kwamba Kinapa tutaweka mikakati ya kuhakikisha kwamba eneo hili linaendelezwa ili liwe sehemu ya utalii katika hifadhi ya taifa ya Kilimanjaro. Tutaweka katika bajeti zetu za hifadhi kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu. Kama unavyoona mahala hapo kuna makorongo, kuna miinuko. Na ili paweze kufikika lazima kuwe na miundombinu. Kwa mfano tutaweza madaraja baadhi ya maeneo,” ameeleza Charles Ngendo.

 

Maelezo ya picha,

Charles Ngendo mhifadhi KINAPA (kulia), Dk Andreas Hemps (wapili kulia ), katikati mwandishi wa BBC Aboubakar Famau

Mti huo wenye umri wa zaidi ya miaka 600 hivi sasa uko chini ya ulinzi wa KINAPA ili kuulinda kutokana na majangili na hata wale wanaotaka kuutumia kama dawa. Mti huo tayari umeingizwa katika rekodi ya dunia kwa kushika nafasi ya sita kwa urefu duniani.

Utafiti wa kuwepo kwa mti huo tayari umewekwa katika mitandao na vituo vya utalii katika nchi mbalimbali duniani, ili kuleta changamoto ya utafiti mwengine utakaoweza kuonesha mti mwengine mrefu katika nchi nyengine yoyote Barani Afrika.

Maelezo ya video,

Safari ya kuufikia mti mrefu zaidi Afrika nchini Tanzania