Thursday, January 16

Balozi Ramia awaaga wafanyakazi Pemba.

WAZIRI wa Fedha na Mipango Zanzibar Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, amewaaga rasmi wafanyakazi wa wizara yake Pemba, huku akiwataka wanafanyakazi hao kutambua kuwa wizara hiyo nimiongoni mwa wizara ngumu pamoja taasisi zake.

Alisema taasisi zilizomo ndani wa wizara hiyo ni ngumu sana, lazima wanapaswa kufahamu kwamba ni kazi za umma na sio zao, hivyo wanapaswa kujitahidi wakati wa kutoa huduma kwa wateja wao.

Waziri huyo aliyaekeza hayo katika sherehe ya wafanyakazi ya kumuaga waziri wao, baada ya kuwahudumia kwa muda mrefu na kufanyika katika ukumbi wa wizara hiyo Gombani.

Alisema lazima wafanyakazi wawe katika mstari mmoja, kufanya kazi kwa uwaminifu, mashirikiano pamoja na kufanya kazi kwa kukinai na kuacha tama.

“Tambuweni Wizara hii kuwa inavishawishi vingi lazima, kama hukinai basi katika wizara hii utaumbuka na kukuweka pabaya katika kazi zako”alisema.

Waziri huyo alisema wizara inamajukumu mawili makubwa, moja ni kuzitafuta pesa popote zilipo na kuziwasilisha katika mfuko mkuu wa Serikali, jukumu la pili amesema kuzigawa kwa malengo yaliokudiwa.

Aliwasisitiza wafanyakazi wa wizara hiyo, kujitahidi kufuata miiko, taratibu za serikali wakati wote wa ufanyaji kazi wao, ili sifa ya wizara hiyo iendelea kuwepo.

Akizungumzia kuelekea uchaguzi mkuu, waziri huyo wa fedha aliwataka wafanyakazi wa wizara hiyo kuhakikisha wanalinda amani ya nchi, na kuacha kujiingiza katika masuala ya siasa wakati wa kazi.

Aidha alizitaka taasisi zinazohusuka na masuala ya ukusanyaji wa kodi, TRA, ZRB, BIMA, PBZ kujitahidi katika ukusanyaji wa mapato, pamoja na kufuatilia kwa kina madeni wanayoyadai kwani serikali inawategemea mapato yake katika kuhudumia wananchi.

Kuhusua dira ya 2020/2050 alisema vijana ndio muhimu kuijuwa dira ya miaka 30 inayokuja, kwani wao ndio wahusika wakubwa katika dira hiyo.

Hata hivyo aliwashukuru wafanyakazi wa wizara yake kwa mashirikiano makubwa waliyompatia wakati wote alipokuwa akiiongoza wizara hiyo.

Mapema afisa mdhamini wa wizara hiyo Pemba, Ibarahim Saleh Juma alimpongeza waziri huyo kwa kuwa nao na kuwafunza mengi, katika muda wake wa utendaji katika wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar.

“Watendaji wa wizara ya fedha wamebadilika sana katika utendaji wao wa kazi, kwa kufuata miongozo yako na hatua kubwa tumepiga ikiwemo kupata makazi bora na mazuri”alisema.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, mdhamini wa TRA Pemba Ibrahim Saleh Juma alisema mapato ya yanayokusanywa na TRA Zanzibar yanabaki katika mfuko wa mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sio kwenda bara.

Aliahidi kufanyakazi kwa bidii katika kipindi chote kinachokuja, ili kuhakikisha lengo la serikali linafikiwa katika ukusanyaji wa mapato.