RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiamewasili Jijini Dodoma leo kwa ajili ya kuhudhuria uzinduzi wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika uwanja wa ndege wa Dodoma, Rais Dk. Hussein amepokewa na viongozi mbali mbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kulizindua Bunge hilo la 12 mnamo majira ya asubuhi hapo kesho Ijumaa.
Kwa kawaida Mkutano wa Kwanza wa Bunge jipya kama huo huwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania analihutubia Bunge kwa maana ya kuweka dira kwenye Serikali yake kwa miaka mitano inayokuja na utekelezaji wa Ilani kadri anavyoona inafaa.
Shughuli hiyo ya uzinduzi wa Bunge itatanguliwa na gwaride maalum ambalo Rais Magufuli atalikagua kabla ya kuingia Bungeni kuhutubi Taifa na kuzindua Bunge.
Rais Magufuli atalihutubia Bunge hilo la 12 ambalo kwa zaidi ya asilimia 90 lina Wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichoshinda kwa kishindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28,2020 wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Ambapo kati ya Majimbo 264 ya Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeshinda Majimbo 256 na kina Wabunge wa Viti Maalumu 94.
Katika safari hiyo, Rais Hussein Mwinyi amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk