Sunday, November 24

Mdhamini aipiga jeki Hard Rock .

AFISA Mdhamini Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Pemba Fatma Hamad Rajab, akimkabidhi mipira, Stoking (Soksi) na seti moja ya Jezi kepteni wa timu ya Hard Rock Emanuel Balele, ambayo ni timu pekee inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar kutoka Kisiwani Pemba.(PICHA NA ABDI SULEIMAN,PEMBA)

 

TIMU ya Hard Rock ndio timu ya pekee kutoka katika kisiwa cha Pemba, kushiriki ligi kuu ya Zanzibar kwa msimu wa mwaka 2020/2021 baada ya kupanda daraja msimu uliopita.

Hard Rock msimu wa ligi 2019/2020 ilishiriki ligi daraja la kwanza Taifa Pemba, ikifanikiwa kurudi ligi kuu ya Zanzibar kwa kishindo baada ya kushuka.

Kutokana na kuwa ni timu ya pekee wadau mbali mbali wa michezo wameanza kujitokeza na kuipiga jeki, ili kuweza kufanya vyema katika ligi hiyo pamoja na kurudi na ubingwa.

Akizungumza na viongozi na wachezaji wa timu hiyo baada ya kuipatia vifaa vya Michezo, kama vile Mipira, jezi na stoking, Afisa Madhamini Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Pemba, Fatma Hamad Rajab, aliwataka wachezaji hao kuongeza bidii katika soka ili kuifanya timu yao kuwa tishio.

Alisema kwa sasa suala la Mpira limekuwa ni ajira kubwa kwa vijana wa mpira wa miguu, aliwasihi kuzidisha kasi na kuwa wawakilishi wazuri wa kisiwa cha Pemba.

“Natambua uwepo wa changamato katika vyama vyetu vya michezo, lakini tunapaswa kutokubeteka tuongeze bidii, lakini pia Rais wetu wa awamu ya nane ameshatuonesha njia katika kuliendeleza soka letu”alisema mdhamini.

Aidh alimshukuru Rais Mstaafu wa Zanzibar kwa awamu ya saba, Dk Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake kubwa za kufufua mpira wa miguu Zanzibar, pamoja na kujenga viwanja vya michezo kiwilaya ambapo Pemba imebahatika kuwa na viwanja viwili.

Alivitaja viwanja hivyo kuwa ni Kishindeni kwa Wilaya ya Micheweni na Kangani kwa wilaya ya Mkoani, huku akiwataka wachezaji kutokujiingiza katika mapenzi, kufanya hivyo kutapelekea kushuka kwa kiwango chao cha Mpira.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Timu ya Hard Rock Mohamed Kway alimshukuru Mdhamini wa Wizara ya Vijana, kwa msaada aliowapatia kuwa sio mdogo kwao katika kipindi hiki cha maandalizi ya ligi kuu ya Zanzibar.

Alisema vifaa hivyo vimefika kwa wakati muwafaka na vitatumiwa kwa lengo lililokusudiwa, huku akiwataka wadau wengine kujitokeza kuisaidia timu hiyo.

Timu ya Hard Rock kwa sasa ndio wawakilishi Pekee kutoka kisiwa cha Pemba kucheza ligi kuu ya zanzibra kwa msimu wa 2020/2021, baada ya timu za Machomanne, Jamhuri, Chipkizi, Mwenge, Selem View kushuka daraja na kucheza ligi daraja la kwanza Taifa Pemba.