Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla ameuagiza Uongozi wa Bodi ya Mapato Zanzibar {ZRB}kuwasilishwa Afisini kwake Ripoti ya Majina ya Wadaiwa sugu wote wa Madeni ya Serikali ndani ya Siku saba ili hatua za kisheria zichukuliwe mara moja dhidi ya wahusika hao.
Alisema wapo baadhi ya Wafanyabishara na Wawekezaji wenye tabia ya kutumia migongo ya Wakubwa kukwepa kulipa Kodi kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizowekwa jambo ambalo huviza ukusanyaji wa Mapato yanayohitajika kuendesha Serikali.
Mheshimiwa Hemed Suleimna Abdalla alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi hapo Makao Makuu ya Bodi ya Mapato Zanzibar yaliyopo Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar kuangalia utendaji kazi wa Taasisi hiyo ya Fedha.
Alisema Bodi ya Mapato Zanzibar ndio tegemeo kubwa la Ukusanyajazi wa Mapato ya Serikali katika kuimarisha Uchumi wake. Hivyo bado ipo kazi kubwa ya kuendelea kukusanya Kodi hasa kwa wale wajanja wanaodaiwa Kodi na hawana dalili wala muelekeo wa kulipa au kupunguza madeni yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba Serikali Kuu haitasita kuwafutia Vibali mara Moja Wawekezaji au Wafanyabiashara wote watakaoonyesha dalili ya usugu wa kulipa Kodi zao kwa mujibu wa Biashara wanazoendesha.
Mapema Meneja wa Madeni wa Bodi ya Mapao Zanzibar Bibi Asya Abisalami alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wapo wadaiwa sugu Zaidi Sita wa Mahoteli na Wafanyabiashara wa Miradi Mikubwa wenye madeni makubwa ya Zaidi ya Shilingi Bilioni 17 yaliyochukuwa muda mrefu.
Bi Asya alisema madeni hayo yamejumuisha pia fedha za baadhi ya Wafanyakazi wa Mahoteli kupitia Michango yao ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii {ZSSF} pamoja na leseni za Biashara.
Naye kwa upande wake Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar Nd. Joseph Abdalla Meza alisema Uongozi wa Bodi ya Mapato Zanzibar umekuwa ukichukuwa hatua mbali mbali za kuhakikisha madeni hayo yanaendelea kulipwa na pale muhusika anavyokaidi maamuzi hayo hufikia hatua ya kufutiwa Leseni yake ya Biashara.
Nd. Meza alisema wapo baadhi ya wadaiwa ambao tayari wamefikishwa kwenye vyombo vya Sheria kuhusiana na kukiuka Mikataba yao ambapo wengine hujiepusha na adhabu kwa kulipa kadri ya masharti wanayowekewa.
Kamishna huyo wa Bodi ya Mapato Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Taasisi hiyo umechukuwa hatua ya kukabiliana na mbinu za baadhi ya Washirika wao kwa kufunga Vifaa vinavyosaidia kuwatabaini baadhi ya Wawekezaji na Wafanyabiashara wanaofuta Taarifa kwenye Mitandao yao.
Alisema Mfumo wa Teknolojia unaotumiwa na ZRB hivi sasa unawezesha kutambua hata Taarifa zilizofichwa au kufutwa na Wateja na hatimae Uongozi huchukuwa hatua ya kumuwajibisha muhusika kwa mujibu wa kosa alilofanya.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/11/2020.