Saturday, October 19

DC Vijana heshimuni mali ya Serekali

 

MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Rashid Hadid Rashid, amesema kuwa kuwepo kwa Programa ya ajira kwa vijana Zanzibar, imekuwa ni mkombozi mkubwa kwa vijana mbali mbali katika kuwainua vijana na kubuni miradi itakayowapatia kipato.

Amesema program hiyo tokea kuanzishwa kwake 2019, chini ya Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo ambayo kwa sasa inajulikana kuwa Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, imekuwa ikiwasaidia vijana kuwapatia vitu vya kujiendelezea na maisha.

Mkuu huyo wa wilaya aliyaeleza hayo mara baada ya kukabidhi boti ya uvuvi kwa vijana wa Misooni, pamoja na vifaa vyake ikiwemo nyavu 10, mashine na maboya kwa lengo la kujiendeleza kimaisha.

Aliwataka vijana hao kuhakikisha wanaitunza na kuithamini boto hiyo, kwani serikali imekuwa ikitumia garama nyingi katika kuwasaidia vijana, huku vijana wakishindwa kuthamini juhidi hizo.

Aidha aliwasihii vijana kuhakikisha wanaitumia boto hiyo kwa shuhuli za uvuvi tu, na sio kwa shuhuli nyengine ambazo sio uvuvi, kwani ikibainika wanaitumia vyengine basi itakua rahisi kuichukua.

“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi sana katika kununulia vifaa vya vijana, sasa vijana munatakiwa kuonyesha ujasiri na ushupavu, katika kuvitumia vifaa kwa lengo lililokusudiwa”alisema.

Alisema serikali ya wilaya haitokuwa tayari kuona boti hiyo, inatumiwa katika usafirishaji wa magendo ya karafuu pamoja na kusafirisha kuni na mkaa.

Hata hivyo aliishukuru serikali ya awamu ya saba chini ya Rais mstaafu Dk.Ali Mohamed Shein, kwa uamuzi wake wa kuanzisha program ya ajira kwa vijana, ambapo sasa vijana wamekuwa wakinufaika na program hiyo.

Kwa upande wake afisa mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba, Fatma Hamad Rajab, alimshukuru Dk.Shein kwa kuanzisha program ya ajira kwa vijana, programa ambayo imekuwa msaada na mkombozi mkubwa kwa vijana nchini.

Alisema wilaya ya Chake Chake imekuwa ni wilaya ya kwanza kunufaika na msaada wa boti ya uvuvi, hivyo vijana wanapaswa kutambua kuwa fedha nyingi zimetumika katika ununuzi wa boto hiyo, jambo ambalo wanapaswa kuthamini na kuitunza.

“hivi ni fedha nyingi sana ambazo zimetumika katika kununulia boti hiyo, vijana munapaswa kuthamini juhudi za serikali ambazo zimezichukua”alisema mdhamini.

Hata hivyo aliwataka vijana hao kuwa wabunifu wakubwa wa vitu mbali mbali, licha ya kuwa ni wavuvi lakini wanapaswa kubuni miradi mengine.

Mwenyekiti wa baraza la Vijana Shehia ya shungi Khalid Khamis Ali, aliahidi msaada huo wa boti kutumika kwa lengo lililokusudiwa ikiwa ni shuhuli za uvuvi.

Aliwataka vijana kuhakikisha wanakua kitu kimoja, katika kuifanya wilaya ya chake chake inaendela kuwa namba moja katika wilaya nne za pemba, katika suala zima la kwuasaidia vijana.