Tuesday, November 26

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar atembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akielezea kutoridhika kwake na baadhi ya Mashine za kukagulia Abiria na Mizigo kutokufanya kazi sawa sawa jambo ambalo ni hatari kwa baadhi ya Watu kutumia mwanya huo kwa mambo maovu.

 

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla amekemea uwepo wa ubovu wa baadhi ya Mashine za kukagulia Abiria na Mizigo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Kisauni jambo ambalo halikubaliki katika eneo hilo muhimu kwa Uchumi wa Taifa.

Alisema changamoto hiyo mbali ya kuzurotesha utoaji wa huduma kwa abiria pamoja na mizigo  lakini pia unaweza kusababisha upatikanaji wa mwanya kwa Wafanyabiashara wenye tabia mbaya ya kuendesha biashara haramu inayoweza kuliingiza Taifa mahali pabaya.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla alitoa kemeo hilo alipofanya ziara fupi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimaitaifa wa Abeid Aman Karume Kisauni na kutoridhika na uwezo wa baadhi ya Mashine zisizofanya kazi wakati Serikali imeshajipanga kuona Uwanja huo unatoa huduma za Kimataifa.

Alisema Viwanja vya Ndege na Bandari ni sura ya Nchi ambayo lazima wageni wanaoingia wapokewe kwa kiwango kinachokubalika hatua inayokwenda sambamba na ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya Taifa.

Alieleza kuwa Viongozi na Watendaji  wanapaswa kuandaa mbinu na mfumo utakaosaidia Serikali iongeze vianzio vyake vya mapato vitakavyoonekana na kuridhiwa moja kwa moja na Wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibainisha kwamba Uwanja wa ndege unahitaji mabadiliko makubwa ili changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi badala ya ile tabia ya baadhi ya Viongozi na Watendaji kusubiri ziara za Viongozi katika maeneo yao.

“ Uwanja wa ndege unahitaji mabadiliko makubwa, mambo yanayowezekana yasisubiri kuongozwa. Na ile tabia ya watendaji kuendelea kuangalia mitandao ya Kijamii Ofisini kwa sasa lazima yaishe”. Alionya Mh. Hemed.

Akizungumzia suala la Mikataba, Mh. Hemed amewaagiza Wanasheria wa Taasisi za Umma kuangalia upya Mikataba iliyotiwa saini katika Miradi iliyoanzishwa kwenye Taasisi zao ili kujihakikishia mapato yanayokusanywa katika miradi ya huduma yanasimamiwa na kukidhi mahitaji halisi.

Alisema ipo baadhi ya Mikataba ndani ya Taasisi za Umma inaonyesha dalili ya uwepo wa mwanya wa rushwa kutokana na kupungua kwa asilimia ya makusanyo ya Mapato ya Serikali ilhali Viongozi wanaosimamia Mikataba wanaendelea kushuhudia hali hiyo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla ameutaka Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuhakikisha haki za kila Mfanyakazi zinapatikana ili kuondosha au kupunguza matatizo yanayowakumba baadhi yao.

Alionya kwamba wapo baadhi ya Watendaji waliofukuzwa kazi kwa tuhuma mbali mbali na baada ya uchunguzi wa kina wameonekana wahana hatia lakini bado wanaendelea kuzunguushwa kitendo ambacho hakitoi haki na Serikali Kuu haitaridhia kuona kinaendelea kuwepo.

Mapema wahandisi wanaosimamia Mashine za Ukaguzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karum walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Baadhi ya Mashine hizo bado zipo kwenye uangalizi wa Kampuni ilizozifunga.

Walisema wakati inapotokezea hitilafu kwa baadhi ya mashine hizo huwasiliana na Wahandisi wa Kampuni hiyo kwa ajili ya kuondosha changamoto pale inapojitokeza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa  Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar Nd. Said Iddi Ndombogani alisema Wafanyakazi wanaosimamia Mashine hizo hupatiwa Leseni baada ya kumaliza mafunzo ya jinsi ya kuzihudumia Mashine hizo.

Hata hivyo, Mkurugenzi Said Iddi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kitengo hicho bado kimekuwa kikikabiliwa na bajeti ndogo inayoshindwa kukidhi mahitaji halisi ya uendeshaji.