Saturday, October 19

Wafanyabiashara kuchukua tahadhari .

WAFANYABIASHARA wa vyakula katika mji wa Chake Chake, wameshauriwa kuendelea kuzitumia ndoo za kunawiya mikono kwa wateja wao, kama ilivyokua kipindi cha ugonjwa COVID 19 ili kuepukana na maradhi mbali mbali ya mripuko kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Ushauri huo umetolewa na Afisa mkaguzi kutoka Baraza la Mji Chake Chake Khamis Abas Machano, wakati alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alipotaka kujuwa mikakati ya baraza hilo kipindi hiki cha mvua.

Alisema kipindi cha ugonjwa wa Covid 19 wafanyabiashara wa mji huo, waliweka madoo nje ya maeneo yao ya biashara na wananchi wakinawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabu, hivyo hali hiyo inapaswa kurudiwa tena kipindi hiki cha mvua.

Aidha aliitaka jamii kushirikiana kwa hali na mali katika kusimamia mji wa chake chake, katika hali ya usafii na kuacha kutupa takataka katika maeneo ambayo hayafai, kwa lengo la kuepuka maradhi ya mripuko ikiwemo kipindupindu.

“Sote tunafahamu kuwa mji wa chake chake ni mji mkubwa, ni kiunganishi cha wilaya nyengine, usafi katika kipindi hiki cha mvua ni muhimu kwa mji wetu huuu”alisema.

Akizungumzia wauza bishara wa kombe, chaza, maandazi, kuhakikisha wanatafuta masanduku maalumu, kwa ajili ya kuhifadhia bidhaa zao kipindi hiki cha mvua zinazoendelea ili kuwanusuru ateja wao na maradhi ya mripuko.

Kwa upande wa mikakati yao walioweka baraza la mji, alisema ni kufanya ukaguzi katika maeneo ya wafanyabiashara wa chake chake, ili kuhakikisha usafi unakuwepo kwa muda wote, huku mkazi zaidi umewekwa katika kipindi cha mvua.

Alisema kesi za makaro zimeongezeka katika maeneo mbali mbali, ili kunusuru maradhi ya mripuko katika kipindi hiki cha mvua zinazonyesha, kwani kumekua na majumba mengi yanatiririsha maji katika majumba yao.

Kwa upande wake msaidizi mkurugenzi maendeleo ya huduma za jamii Ali Makame Mdungi, aliwataka wananchi kuzingatia umuhimu wa kulinda mazingira, ili kuepuka kupata maradhi ya mripuko.

Alisema jukumu la kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yaliyowazunguruka, sio la baraza la mji chake chake pekee bali ni jukumu la kila mtu kuhakikisha anaweka mazingira safi katika maeneo yake.

“Nivizuri wananchi katika kipindi hiki kuyatumia kikamilifu madampo yaliyojengwa katika maeneo yao kwa kuhifadhia takataka, kuliko takataka kutupa nje na kusababisha uchafuzi wa mazingira”alifahamisha.

Aidha aliongeza kuwa mikakati yao kwa sasa ni kusafisha mitaro mikubwa ya maji, mitaro wenyewe ni wa kichungwani, Msingini, Mtoni na miembeni, ili maji ya mvua yaweze kupita bila usumbufu wowote.

Kwa upande wao wafanyabiashara wa vyakula katika maeneo ya mji wa Chake Chake, wamesema kuwa tayari wameshaanza kuweka mazingira sawa katika ameneo yao ya mikahawa.

Wamesema suala la usafi katika maeneo ya vyakula ni jambo la muhimu sana, hususana katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea.

“Kuna baadhi ya wateja wanafika kutaka chakula kwa kuvutiwa na mazingira mazuri ya utayarishaji, mpaka utoaji wa huduma zikiwa safi, lazima biashara yako uipende kwa hali yoyote ile”alisema.