Saturday, October 19

ZAC yazidi kupambana na maambukizi ya Ukimwi.

NA SALIM TALIB, PEMBA.

 

 

NA SALIM TALIB, PEMBA.

OFISA Mdhamini Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salim, ameipongeza Tume ya UKIMWI Zanzibar kwa juhudi kubwa wanazozichukua za kupambana na maradhi hayo, ambapo tafiti za mwaka 2016-2017 kuonesha watu walioathirika ni 0.4% Unguja na 0.2% Pemba.

Alisema, ni vyema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikishirikiana na tume hiyo kuendelea kuchukua jitihada zaidi katika kupambana na janga hilo hadi kufikia kuyamaliza kabisa kwa kufikia asilimia 0.0%.

Aliyasema hayo wakati alipokua kizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Baraza la Mji Chake chake katika Bonanza la maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Kiwilaya lililofanyika katika kiwanja cha Polisi Madungu Wilaya ya Chake Chake.

Alifahamisha kuwa, jamii ifahamu kwamba maradhi ya UKIMWI bado yapo hivyo aliitaka jamii kuwa makini na kujitambuwa hususani vijana kwani alisema wao ndio nguzo ya Taifa.

“Ni imani yangu kutokana na kasi ya utendaji kazi wa Tume ya UKIMWI pamoja na utoaji elimu kwa jamii maradhi haya yataondoka kabisa na Zanzibar itabaki salama kwani Zanzibar bila ya UKIMWI inawezekana” alisema.

Alieleza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua ikishirikiana na nchi mbali mbali Duniani katika kuadhimisha siku ya UKIMWI lengo lake likiwa ni kupambana na janga hilo na kulimaliza kabisa.

Alisema, Serikali inajitahidi kuweka miundo mbinu mbali mbali ikiwemo ujasiriamali kwa rika tofauti ili vijana wajishughulishe kiuchumi huku wakijiepusha na vishawishi vitakavyo sababisha kujiingiza katika matendo maovu.

Mkurugenzi Tume ya UKIMWI Zanzibar Dk. Ahmed Mohamed Khatib alisema, lengo kuu la bonanza hilo ni kukumbushana kuwa maradhi ya UKIMWI bado yapo kwani tafiti zinaonesha ugonjwa huo bado unaathiri maisha ya binaadamu.

“Tumefarijika kuona wananchi wamejitokeza kwa wingi kupima afya zao katika bonanza hili wananchi 135 leo wamepimwa jambo ambalo linatupa moyo wa kuwa jamii inathamini juhudi zetu” alisema.

Alisema, kuna haja ya jamii kupeana taaluma juu ya ugonjwa huo hususani kwa vijana kwani wana uelewa mdogo dhidi ya maradhi ya UKIMWI jambo ambalo linapelekea kufikia 250 kwa mwaka.

Akisoma risala kwa niaba ya ZAPHA+ Maryam Said Abdalla alisema, waathirika wa janga hilo wamekua wakikabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kuongezeka kwa masharti magumu kwa misaada inayotolewa na wafadhili, hali ngumu ya maisha na lishe duni kwa watu wanaoishi na VVU.

Hafidh Juma Iddi mkaazi wa Minazini Chake chake ambae alishiriki katika zoezi la upimaji UKIMWI katika bonanza hilo alisema, fursa hiyo imempa faraja kubwa kwani amejua afya yake ambayo itapelekea kuishi bila wasi wasi.

Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani huadhimishwa kila ifikapo Disemba 1 ya kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema“TUSHIKAMANE NA TUWAJIBIKE KUMALIZA UKIMWI DUNIANI”