Saturday, October 19

Jamii itambue umuhimu wa kuwafahamisha watoto kujikinga na maradhi ya mripuko.

 

HABIBA ZARALI,PEMBA.

JAMII kisiwani Pemba imetakiwa kutambuwa umuhimu wa kuwafahamisha watoto wao, jinsi ya kujikinga na maradhi ya mripuko hasa katika kipindi hichi cha mvua kinachoendelea.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi  kwa nyakati tofauti wazazi na walezi kisiwani hapa, walisema katika maisha ya kila siku, ni vyema wazazi kuanzisha wigo wa mashirikiano katika malezi bora, ili watoto waweze kutambua na kutekeleza mambo mema yenye maslahi kwa maisha yao.

Walisema kuwahimiza watoto kujuwa umuhimu wa afya  njema na kujikinga ma maradhi si ya madaktari peke yao, badala yake hata wazazi wana nafasi hiyo ambayo ni moja kati ya njia za kuwafikisha pahala pazuri katika maisha yao ya kila siku.

Salma Suleiman  mkaazi wa Mkoani, alisema kutokana na athari kubwa inayosababishwa na maradhi ya mripuko, ni vyema kila mzazi kuhakikisha anakaa na watoto wake kuwaelekeza kuhusu kujiepusha na maradhi hayo, ikiwemo kuchezea maji machafu na kula chakula kisicho salama.

Alisema iwapo wazazi watawapa elimu hiyo watoto wao kikamilifu, bila shaka wataweza kuelimika na kutekeleza na hata kuwafundisha wenzao hasa ukizingatia watoto wanauelewa wa haraka wakielimishwa.

“unapokuwa na ujumbe unataka ufike pahala wewe mpe mtoto tu utafika mara moja, sasa na wazazi wasijikalie peke yao lakini na wawape watoto elimu hiyo”,alisema.

Saumu Juma mkaazi wa Mtambile, alisema bado wazazi wana jukumu la kutowa elimu mbalimbali ya kujikinga na maradhi ya mripuko kwa watoto wao, ili waweze kuepukana na mripuko wa maradhi hayo.

Alisema wapo baadhi ya wazazi wana tabia ya kuwapenda watoto wao  mapenzi ya kupindukia, hawawezi kuwakataza lolote hata suala la kuhatarisha maisha yao kiafya, jambo ambalo linaipeleka jamii pahala pabaya.

Alifafanua kuwa suala la muhali kwa wazazi ni baya katika jamii kwani linaongeza kizazi kisicho na heshima wala maadili na kuongeza urithi mbaya wa ukaidi.

Nae Mohamed Kombo Ali alisema watoto wanahitaji sana elimu ya afya, ili iweze kuwaokowa na maradhi mbalimbali yakiwemo ya mripuko ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Akizungumzia kuhusu ushirikiano wa wazazi katika malezi bora  katika dini, Zahor shaaban mkaazi wa Chakechake alisema ushirikiano wa wazee kwa kuwahimiza watoto mambo mema umehimizwa hivyo ni vyema kufanya hivyo, ili jamii iweze kuwa salama .

Alisema watoto ni vyema wakasomeshwa elimu zote ikiwemo ya dini na hata ya dunia kwani inawapelekea kujuwa mambo mengi na kujifunza yanayowahusu.

Nae Khadija Ally Yussuf mkaazi wa Mkanyageni alisema watoto wanahitaji kupatiwa elimu wakiwa wadogo, ili waweze kuelewa na mapema wajibu wao ikiwemo umuhimu wa afya njema na kujiepusha na maradhi.

Hivyo aliwataka watoto kuendelea kusikiliza mafundisho yote wanayopewa na wazazi wao, ili waweze kupata faida katika maisha yao.