Saturday, October 19

Jamii yatambuweni maradhi yasiyopewa kipaumbele.

 

NA MARYAM SALUM, PEMBA.

JAMII Kisiwani Pemba imetakiwa kutambua yapo maradhi yasiyopewa kipaombele, ambayo yanaweza kumpata kila mtu na kila rika, hivyo ni vyema kuchukua tahadhari, katika kujikinga na maradhi hayo.

Hayo yalielezwa na Mratibu wa kitengo cha maradhi yasiyopewa kipaombele Kisiwani Pemba, Dk Saleh Juma Mohamed wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Mkoroshoni Chake Chake.

Alisema wananchi waliowengi hufikiria kwamba maradhi hayo huwapata watoto wadogo tu, jambo ambalo sio sahihi kwani maradhi hayo huwapata watu wa rika lolote.

“Watoto wadogo ndio wanaonekana kupatwa na maradhi ya mripuko, kwa sababu ndio ambao wanaonekana mara nyingi kucheza ama kuzurura ovyo, kwenye mazingira yasiyokuwa salama juu ya afya zao,” alisema Mratibu huyo.

Alisema kuwa maradhi haya yameitwa maradhi yasiyopewa kipaombele kwa sababu, ni maradhi yanayotoka nchi za joto, huku jamii inachukulia hayana umuhimu wala hawashuhuliki.

“Maradhi haya tumeita jina hilo kwa sababu watu hawayashuhulikii wala hawana habari nayo kutokana na kuwa linachukua muda mrefu, bila kuonekana kwa athari kwa vile lipo hivyo jamii inakuwa ikizarau, bila kujua ni athari gani zinaweza kuwepo,” alifahamisha Mratibu.

Akitolea mfano, alisema mtu anapofuatwa kutakiwa kula dawa za kichocho, mara nyingi majibu yanayopatikana kitoka kwa jamii husema kwamba kichocho huwapata watoto wadogo, kitu ambacho sio kweli kabisa hicho kwa sasa.

Alifahamisha katika harakati za mtu mara nyingi zipo kwenye maji, shughuli nyingi zinazofanyika ni kwenye maji kwa njia yoyote, bila kujua kwamba hayo maji yameshaathirika ama vipi.

“Isitoshe kitaalamu wadudu wa maradhi ya Kichocho wanakuwa na uwezo wa kuishi ndani ya mwili wa binaadamu zaidi ya miaka ishirini,” alieleza mratibu huyo.

Aliyataja maradhi yasiyopewa kipaombele ni pamoja na Kichocho, Matende, Vikope, pamoja Minyoo klwa Zanzibar, ingawa yapo mengine lakini kwa hayo ndio yanayofahamika zaidi.

Alieleza kuwa, kutokana na tayari wadudu wameshaishi muda mrefu katika mwili wa binaadam, ndipo baada ya muda hali inaanza kubadilika na kuonyesha zile athari, hapo mtu hupoteza maisha kutokana na kua tayari wadudu wameshachamuathiri.

Akizungumzia juu ya maradhi ya Minyoo, alisema maradhi ya minyoo na Kichocho, wadudu wake wanauwezo wa kuishi ndani ya mwili wa binaadamu kwa muda wa wiki mbili hadi tatu, ndipo dalili zake zinaweza  kujitokeza.

Maradhi ya matende yanatokana na mbu aina ya (Ukiros)wanaishi  kwenye makaro na majaa, wakati akimtafuna mtu athari zake hubaki juu ya ngozi, bila kufikia ndani zaidi ni tofauti na athari ya mbu wa malaria.

“Kwa muda wa mwaka mzima huwezi kuona dalili yoyote, ambapo hata ukijikugundua dalili zake tayari mtu ameshapata maambukizi hayo,”alieleza.

Akizungumzia suala la chanjo, alisema hadi sasa hakuna chanjo yoyote ya kuweza kuzuia sumu ya maambukizi ya mbu hao wa mateende, katika kukinga afya ya binaadamu.

Kuhusu maradhi ya vikope, alisema maradhi hayo mara nyingi hutokezea katika ukanda wa Micheweni, hiyo inatokana na hali ya mazingira waliyonayo, ikiwemo mazingira ya vumbi na kusababisha kupatikana kwa maradhi hayo.

Hata hivyo alisema kitengo chao kiliweza kufanikiwa kutoa elimu kwa jamii juu ya kupambana na maradhi yenye kuambukiza, kwa kutoa dawa mbali mbali kwa jamii ikiwemo Micheweni.

Aidha aliwataka wananchi kuchukuwa tahadhari katika kipindi cha mvua za vuli, kwenye usafi, kwa watoto na kwenye mazingira mengine, kwani mripuko sio minyoo pekee wala Kichocho, pia ipo kolera ni hatari zaidi, hivyo kutumia maji safi ni jambo la