Saturday, October 19

WANAFUNZI wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) tawi la Pemba, waishauri Ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali Zanzibar

 

WANAFUNZI wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) tawi la Pemba, wameishauri Ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali Zanzibar kuendelea kutoa elimu ya sheria kwa jamii, ili iweze kufahamu haki zao na namna ya umiliki na matumizi ya ardhi.

Walisema, kumekua kukijitokeza migogoro mingi mitaani ambapo baadhi ya watu hujimilikisha ardhi kinyume na sheria, lakini kuwepo kwa sheria hiyo kutawezesha kutatua changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa.

Waliyasema hayo, wakati walipokua akizungumza na mwandishi wa habari mara baada ya kupatiwa mafunzo ya elimu ya sheria huko katika ukumbi wa chuo hicho mjini Chake chake.

Kwa upande wake, mwanafunzi katika ngazi ya Diploma Juma Suleiman Hamad, alisema elimu ya sheria inahitajika kwa jamii kwani bado haina uwelewa kuhusiana na sheria ya umiliki na matumizi ya ardhi, ambapo watu hurithishana ardhi kinyume na utaratibu.

“Mimi nashukuru kwa kupata mafunzo haya yamenifanya nijue sheria ya umiliki na matumizi ya ardhi kiukweli ni mazuri kwani tumekua tukiona migogoro ya ardhi ambayo inajitokeza sana mitaani lakini kuwepo kwa sheria hii nimejua kwamba tumekua tukifanya makosa” alisema.

Alieleza kuwa, jamii haitambui haki ya matumizi ya ardhi na haina uwelewa kwamba bodi ya uhaulishaji ardhi ndio inayosimamia masuala mazima ya urithishaji na ndio sababu ya kurithishana ardhi kinyume na sheria.

Naibu waziri wa Elimu Afya na Mazingira wa chuo hicho, Adhra Asaa Hamad, alisema chuo hicho kimefarijika kupatiwa mafunzo hayo kwani wataweza kujua haki zao za msingi katika jamii ambazo zitawasaidia kuweza kudai haki zao.

“Tumekua tukiona watu wanavo rithishana mali kwa kutofuata sheria lakini kwa kupitia mafunzo haya naamini tutaitumia vizuri elimu hii kwa kuwafikishia wengine huko mitaani kwetu” alisema.

Aidha, aliishauri ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu hiyo mijini na vijijini ili kuifanya Zanzibar kuwa sehemu salama.

Nae Mwanafunzi Ali Suleiman Daudi alisema, amejifunza sheria na baadhi ya haki ambazo mwananchi anatakiwa kuzipata, hivyo aliomba ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali kwa mara nyengine kuweza kuwafikia chuoni kwao na kuwapatia elimu za sheria.

Akiwasilisha mada ya umiliki na matumizi ya ardhi Mwanasheria mwandamizi na mkuu wa kitengo cha usimamizi wa kesi, kutoka Ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali Ali Hassan Ame alisema, mbali ya kuwepo sheria maalumu inayohusu matumizi na umiliki wa ardhi kuna sheria kadhaa zinazohusiana na ardhi.

Alisema, miongoni mwa Sheria hizo ni pamoja na sheria ya kumtabua mtumiaji wa ardhi, sheria ya usajili wa ardhi, uhaulishaji ardhi, kukuza na kulinda uwekezaji Zanzibar, sheria ya upimaji ardhi, sheria ya mahakama ya ardhi na sheria ya milikipacha.