Saturday, October 19

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Uchumi na Uwekezaji, Mhe Mudrick Ramadhan Soraga anena.

 

Na Mwandishi wetu

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Uchumi na Uwekezaji, Mhe Mudrick Ramadhan Soraga amesema kuwa hatokuwa tayari kutumbuliwa kwa makosa ya uzembe yatakayofanywa na wasaidizi wake.
Kauli hiyo ameitowa katika kikao cha pamoja cha watendaji wa wizara yake kilichofanyika Mwanakwerekwe mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alisema kuwa wanaingia katika Serikali ya awamu ya nane kwa kila Mtendaji atambuwe majukumu yake, ili kuendana na Kasi ya Rais wao.
Hivyo awe Mkurugenzi, Katibu Hata msaidizi ambae atakuwa haendani na Kasi hiyo hatomuonea haya na badala yake atamuandikia barua ya kuomba kuondolewa ili awapishe wenzake wanaoendana na kasi hiyo.
Sambamba na hiyo aliwataka watendaji hao kila mmoja atimize wajibu wake ili kuweza kufanikisha malengo ya wizara ambayo yamewekewa na Rais.
“Mimi sitokubali kuja kutumbuliwa Kama nitaona Mkurugenzi hunifai, unanichelewesha safari yangu nakupa kazi huitekelezi kwa muda ninaouhitaji nitakusamehe”, alisema.
Hivyo alisema lazima waende na ile Kasi ambayo ameitaka Rais ambayo iwe ni kwa mpangilio na sio kwa kusukumiza mambo.
Hivyo aliwataka wawe makini katika utekelezaji wa majukumu yao na kwa haraka zaidi na kuondoa sababu zisizokuwa na msingi.