Saturday, October 19

Makamo wa Rais wa Zanzibar atua Pemba.

 

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, amewapongeza wananchi wa mikoa miwili ya Pemba, kwa mapokezi yao mazuri kwani hali hiyo inaonyesha heshima kubwa kwa Rais Dk Hussein Mwinyi kumuamini katika utendaji wake wa kazi.

Alisema Tayari Rais ameshaanza kupanga serikali yake na mwelekeo wa serikali hiyo ya awamu ya nane, kila mtu ameshaanza kuona kwani Imekusudia kuwabadilisha wananchi wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi wa mikoa miwili ya Pemba, mara baada ya kuwasili Kisiwani hapa kwa mara ya kwanza tokea kuteuliwa kwake na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi.

Alisema kasi ya serikali hiyo imeanza hivyo mashirikiano na uwajibikaji ndio kitu muhimu, kwani hawako tayari kuona wabadhilifu, wazembe na walarushwa kupata nafasi katika serikali hiyoo.

“Kila mtu afanyekazi kwa wajibu wake, watendaji wanaodhorotesha maendeleo watafichuliwa na hatokuwa tayari kuona maendeleo yanarudishwa nyuma, popote walipo watafichuliwa na kushuhulikiwa”alisema.

Aidha alisema kila mwananchi na mfanyakazi anapaswa kutimiza wajibu wake, kwani suala la uwajibikaji linamgusa kila mtu kwa nafasi yake, hivyo kila mtendaji anapaswa kuwajibika kikamilifu.

Hata hivyo aliwataka kutambua kuwa nafasi aliyonayo ni ya wazanzibari wote, aliahidi kufanya kazi kwavitendo ili wananchi wa Zanzibar waweze kupata amendeleo bora.

Kwa upande wake waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk.Khalid Sulum Mohamed alihidi kuwa mwadilifu na kufanya kazi kwa kwendana na spidi za viongozi wa serikali walipo madarakani.

Kwa upande wake waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Simai Mohamed Said, amesema kuwa yeye hatokuwa tayari kuwa waziri wa kwanza kuondoshwa madarakani hiyo watendaji wanapaswa kuwa tayari kuacha kufanya kazi kimazowea.

Alisema kwa sasa amekuwa waziri wa kwanza kufika kisiwani Pemba, kuanza ziara ya kutembelea miradi mbali mbali iliyoko kwenye Wizara ya Elimu.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Omar Khamis Othaman, aliwashukuru wananchi wamikoa miwili ya Pemba, kwa kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Aliwataka wananchi kuendana na kasi iliyopo ya viongozi walioteuliwa na Serikali, ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya nane.