Saturday, October 19

Jamii iendelee kudumisha amani na utulivu nchini.

 

WADAU wa uchaguzi Kisiwani Pemba wametakiwa kuishajihisha jamii kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini katika kipindi hichi ambacho Taifa linatoka katika uchaguzi mkuu.

Uchaguzi umemaliza na serikali iko madarakani hivyo lililopo kwa sasa ni kudumisha amani na utulivu na kusahau yaliyopita kwani ukizingatia kuna maisha baada ya uchaguzi.

Akitowa mada juu  umuhimu wa kulinda amani kwa wadau hao uliofanyika ukumbi wa Maktaba Chake chake kaimu mratibu wa kituo cha huduma za sheria tawi a Pemba Safia Saleh Sultan alisema kila mmoja ana haki ya kulinda amani na kuondosha ugomvi ,vita na mifarakano katika nchi ili kila mmoja aweze kuendesha maisha kwa salama .

Alifahamisha kuwa ili amani iweze kudumu vyema ni vizuri kuanzia ndani ya familia na baadae kwenye shehia, wilaya , mikoa na nchi mzima kwa lengo la kila mmoja kupata haki yake stahiki.

“Kila mtu anahitaji kupata ulinzi wa amani na hakuna anaehitaji kuikosa hivyo ni vyema kila mmoja atunze haki hiyo ili nae aipate kama wenzake,”alisema.

Akizungumza wajibu wa raia katika kutunza amani alisema, kwanza waweze kujitambuwa wao wenyewe na kujuwa sheria ya Serikali  ya utawala uliopo.

Alisema ni vyema kila mmoja kufuata sheria zilizowekwa ambazo zinakwenda sambamba na utawala bora na kutekeleza wajibu wao ili kila mmoja aweze kupata haki yake.

Akizungumzia wajibu wa vyombo vya habari katika kutunza amani Safia alisema, wataweza kutunza amani  kupitia kalamu na sauti zao kwa kufanya usawa katika kazi zao.

Kwa upande wa vyombo vya ulinzi alisema, vina jukumu kubwa kisheria la kulinda amani  ya nchi ikiwemo raia na mali zao hivyo ni vyema kuwa na uwajibikaji,uhalali,usawa na ulazima.

Mapema akifunguwa mkutano huo Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Pemba ( PPC) Bakar Mussa Juma alisema ni jukumu la waandishi wa habari kuifanya jamii kuwa kitu kimoja kwa kuandaa habari ,vipindi na makala zitakazoelimisha kuhusu amani ya nchi yao.


Alisema waandishi wa habari ni mawakala wa amani hivyo wanapaswa kuishajiisha jamii kwa kupitia taaluma yao juu ya umuhimu wa kudumisha amani na utulivu kwani bila amani hakuna linaloweza kufanyika.

Aliwataka  kuelewa  kuwa wao ni sauti za wale wasio na sauti hivyo wanawajibu wakufanya kazi zao kwa  kuzingatia maadili ya kazi zao ili kila mmoja katika jamii waweze kumtendea  haki na usawa.

“Katika kipindi hichi kidogo cha uchaguzi kilichopita kama binaadamu tunatakiwa kusahau yote yaliyopita hata kama watu walikwaruzana na sasa tuendeleze mbele amani kwani kuna maisha baada ya uchaguzi,”alisema.

Nae Mwenyekiti mstaafu wa klabu hiyo Saidi Mohamed Ali alisema ,kila kitu kina wakati wake  na ratiba ya jambo lolote linahitajiwa kufuatwa hivyo kilichosababisha kufanywa uchaguzi kimeshatimia hivyo watu waangalie maisha kwa sasa.

Alifahamisha kuwa iwapo ikitokezea kuna  mivutano ni vyema ikawa ni yenye kujenga sio yenye kubomoa kwani hakutaweza kuwa na maisha mazuri kama ikijitokeza mifarakano katika jamii.

Nae Sada Abubakar Khamis kutoka kitengo cha mrajis wa NGOs akitowa shukrani zake kwa klabu hiyo aliwataka wadau hao kuwa wawakilishi kwa wengine kwani lengo ni kusonga mbele na sio kurudi nyuma.

Alisema hakuna mbadala wa amani katika nchi na kusisitiza kuwa ni rahisi kuivunja lakini ni tabu kuirejesha hivyo kila mmoja anatakiwa kuchukuwa jitihada za makusudi kuhakikisha anaidumisha amani nchini.

Kwa upande  wa wadau waliopata mafunzo hayo walisema ili kuwepo na amani lazima kuwepo na haki hivyo suala la kutunza amani ni la wote na lisiangaliwe kwa baadhi ya watu pekee.

Mkutano huo ulioandaliwa na Pemba Press Club (PPC) kwa kushirikiana na inter news, USAID na fHi360 uliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari,wanasiasa, wanasheria, vikosi vya ulinzi na usalama, viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali na binafsi .