Saturday, October 19

Makamo wa Pili awajia juu wakandarasi ZRB na ZBC.

 

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, amewaonya wakandarasi wanaojenga jingo la Ofisi za ZRB Gombani na Ofisi za ZBC TV Mkoroshoni, kuacha tabia ya kutafuta sababu ya kwamba mvua ndio kigezo kilichopeleka kuchelewa kwa majengo hayo kumalizika kwa wakati.

Alisema tabia hiyo ya wakandarasi wanapopewa kazi za ujenzi kwa majengo ya serikali mwisho wake umefika, bali wanapaswa kujega kulingana na mikataba ya ujenzi waliosainiana na wenyeji wao.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, alitoa kauli hiyo baada ya kutembelea majengo hayo kwa nyakati tafauti, katika mwendelezo wa Ziara yake Kisiwani Pemba.

Akizungumzia jingo la Ofisi za ZRB Gombani, alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha jingo hilo analimaliza ndani ya muda uliopangwa, wakati waliposaini mikataba ya ujenzi vyenginevyo itakuwa ndio kazi yake ya mwisho kupewa kwa Zanzibar.

“Kipindi ulipokuwa unasaini mimi nilikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba na nilishuhudia, ulijikubalisha utajenga hata kama kutakua na mvua au jua, sasa visingizio vya mvua havina nafasi katika serikali hii”alisema.

Alimtaka kamishana wa bodi ya Mapato Zanzibar ZRB Joseph Abdalla Meza, kuhakikisha anambana mkandarasi pamoja na kufuata taratibu za mikataba ya ujenzi, ili jengo liweze kumalizika kwa wakati muwafaka, na wafanyakazi waweze kufanya kazi zao kwa urahisi sana.

“Rais Mstaafu aliweka jiwe la msingi jingo hili, maneno hayo yote hayo ya mvua hayakuwepo sasa leo hii kauli haikubaliki, lazima ujenzi huu umalizike kwa wakati muwafaka”alisema Makamu wa Pili.

Akizungumzia ujenzi wa jengo la ZBC mkoroshoni, alisema haipendezi kutumia visababu katika masuala ya ujenzi, kwani ZBC wanashida na sehemu za makaazi ndio maana serikali ikaamua kujenga jengo hilo.

Alisema kwa sasa miezi mitatu imezidi ya ujenzi kutokukamilika, huku asilimia 80% ya fedha za ujenzi zilipwa na jengo liko asilimia 75%, alimtaka kutokutumia fursa ya kuzorotesha ujenzi huo, serikali haitomvumilia mkandarasi yoyote katika kipindi hiki cha awamu ya nane ya serikali.

Alimtaka mkandarasi wajengo la ZBC kuhakikisha milango 30 iliyokuwa tayari ipachikwe haraka iwezekanvyo, pamoja na iliyobakia ifikishwe kwenye jengo husika.

Kwa upande wake mkandarasi wa ujenzi wa jengo la ZBC TV Mkoroshoni, Injinia SP Juma Makame alisema ujenzi huo mkataba wake ni miezi 18 lakini walikubali kulijenga kwa miezi 12, lakini tatizo kubwa kwao ni upatikanaji wafedha.

Alisema kuwa kazi hiyo itaweza kumalizika kulingana na upatikanaji wa fedha, hivyo aliahidi kwamba watahakikisha wanakwenda na kasi ili kumaliza kwa wakati.

Knaye Mkandarasi kutoka kampuni ya Advent Consternation Franc Mohan, alisema changamoto kubwa iliyopelekea kutokumalizka kwa wakati ni kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikishenya, ambapo kwa sasa watahakikisha wanamaliza ndani ya muda na kuweza kufunguliwa.