Sunday, October 20

Mbunge wa Kiwani Rashid Abdalla Rashid, amekabidhi gari la kubebea wagonjwa (AMBULANCE).

MBUNGE wa Jimbo la Kiwani Wilaya ya Mkoani Rashid Abdalla Rashdi (kushoto) akimkabidhi ufunguo wa gari ya kuwabeba wagonjwa ya jimbo hilo, katibu wa CCM mkoa wa Kusini Pemba Mohamed Ali Khalfa, ikiwa ni miongoni mwa ahadi alizozitoa kwa wananchi wajimbo hilo wakati wa kuomba kura.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

NDANI ya siku 20 tokea kula kiapo Bungeni, hatimae mbunge wa Jimbo la Kiwani Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba Rashid Abdalla Rashid, amekabidhi gari la kubebea wagonjwa (AMBULANCE) kwa wananchi wa jimbo hilo likiwa na thamani ya shilingi Milioni 32,000,000/=.

Gari gilo ambalo litaweza kutoa huduma kwa kuwafikisha wagonjwa katika vituo vya afya kwa lengo la kupata huduma za matibabu pale wanapopatwa na tatizo.

Akizungumza katika makabidhiano ya gari hilo kwenye uwanja wa mpira Mauwani, mbunge huyo alisema CCM ikiahidi inatekeleza tena kwa vitendo na sio kumumunya maneno.

Alisema kwanza ameanza na sekta ya afya ambayo ndio sekta muhimu katika jamii, kwani gari hiyo itatoa huduma katika shehia zote zilizomo ndani ya jimbo hilo.

“Katika Jimbo letu kuna vikundi vingi na tayari tumeshatoa, tumeshawataka wanavikundi kuvioredhesha tuvijuwe ili tuweza kuona wapi tunawasaidi”alisema.

Aidha alisema tayari kuna vyarahani 35 vipo kwa ajili ya kuwapatia wanavikundi vya ushoni, vilivyomo ndani ya jimbo hilo ili kujikomboa na umaskini.

Kwa upande wake katibu wa CCM mkoa wa Kusini Pemba Mohamed Ali Khalfan, alimpongeza mbunge wa jimbo hilo kwa uamuzi wake wa haraka wa kutekeleza kwa vitendo ahadi yake ya grari la wagonjwa.

Alisema viongozi wa CCM waliochaguliwa majimboni wanapaswa kutekeleza kwa vitendo ahadi zote walizozitoa kwa wananchi wakati wakiwaomba kura, chini ya usimamizi wa chama cha Mapinduzi.

“Masheha kila baada ya miezi mitatu wametakiwa kupeleka ripoti ya utekelezaji wa ilani kwenye matawi, madiwani wawakilishi na wabunge kila mtu ametakiwa kufanya hivyo, chama kinataka kuona viongozi wamefanya nini kwa wananchi”alisema.

Alisema katika awamu hii hakutakuwa na madudu katika miradi ya maendeleo, wapiga pesa na madili hawatokuwa na nafasi yoyote, chama kimeahidi na kimetekeleza kwa vitendo.

Aidha aliwataka wananchi kutambua kuwa gari hiyo ya kubebea wagonjwa ni yao, wala gari hiyo haina itikadi ya chama chochote wala dini.

Naoi baadhi ya wananchi wa jimbo hilo, wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mbunge huyo ameweza kutekeleza kwa vitendo ahadi zake, kwani waliotangulia hawakuwahi kufanya kitu.

Ali Talib Abdalla alisema mbunge huyo ameweza kuonyesha kuwa na nia njema na wapiga kura wake, katika suala la upikaji kura ilikuwa ni siri, hivyo wananchi wanapaswa kutambua kuwa maendeleo hayana chama.

Aliwataka viongozi watakaokabidhiwa dhamana za gari hiyo, kuhakikisha wanalitunza na kuithamini gari hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Bahati Abdalla Suleiman alimpongeza mbunge huyo kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zake, kwani gari hiyo itaweza kuwasaidia sana akinamama wanapopata na matatizo hususana wakati wa kujifungua.