Saturday, December 28

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar: Vijana kuanzia sasa tieni nia ya kukataa kuwa waathirika wa Virusi vya Ukimwi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akihutubia katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar leo 1 Disemba 2020.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwataka Vijana kuanzia sasa watie nia ya kukataa kuwa waathirika wa Virusi vya Ukimwi, Jamii lazima ishirikiane kulilinda kundi hilo ili liendelee kubakia salama.

Alisema utafiti unaonyesha kuwa Vijana wenye umri baina ya miaka 15 hadi 24 bado wanaongoza katika kupata maambukizo mapya ya Virusi vya Ukimwi kila Mwaka kwa asilimia 50% ya Watu wote changamoto ambayo jitihada za makusudi zinahitajika katika kupambana nayo.

Akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani  hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema bila ya kuwa na Vijana wenye Afya nzuri, wachapa Kazi, ile dhamira ya Serikali isemayo yajayo ni neema tupu itabakia kuwa ndoto tupu.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema mapambano dhidi ya maambukizo ya Virusi vya Ukimwi yanahitaji ushiriki wa kila Sekta kama ilivyojidhihirisha wakati wa mapambano dhidi ya Homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona.

“ Tumeshuhudia kuwepo kwa mashirikiano ya Mataifa katika kukabiliana na Corona yaliyoonyesha kwamba Taifa haliwezi kuwa salama kama Taifa jengine haliko salama. Mshikamano huu pia unahitajika katika kumaliza virusi vya Ukimwi Duniani”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

 

Alieleza kwamba maeneo ya Kazi  kwa bahati mbaya bado yanaviashiria vya kuwepo uwezekano wa Watu kuambukizwa Virusi vya Ukimwi, lakini juhudi za kuzuia maambukizo hayo haziendani na ukubwa  wa viashiria hivyo. Hivyo ni vyema ikawepo mipango itakayoyaweka maeneo hayo salama.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka Viongozi wa Taasisi za Serikali na hata zile binafsi kutenga fedha kwa shughuli za kupambana na Ukimwi katika Mipango ya Kazi na kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa ili zitumike kwa lengo husika.

Mheshimiwa Hemed aliwapongeza Viongozi wa ngazi za Mikoa, Halmashauri, Mabaraza ya Miji na Manispaa kwa kufanikisha Kampeni  ya Kijana Kataa Ukimwi iliyokuwa chachu ya kuwashajiisha na kuwahamasisha Vijana na Wananchi kupima Afya na kupata Elimu juu ya Maradhi ya Ukimwi.

“ Kampeni hii iliambatana na mashindano mbali mbali kama mechi za mipira ya miguu, makongamano, uhamasishaji kupitia vyombo vya Habari, maonyesho ya Magari Mitaani  yaliyopita katika maeneo mbali mbali”. Alisema Mh. Hemed.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Washirika wake wa Maendeleo imepata mafanikio makubwa  katika kupambana na maradhi hayo tokea yalipoingia Nchini mnamo Mwaka 1986 na kudhibitiwa kubakia kuwa chini ya asilimia 1% kwa kipindi cha Miaka 34 sasa.

Mh. Hemed alibainisha kwamba Zanzibar kwa mujibu wa Taarifa za Wataalamu ina asilimai 0.4% ya Watu ambao wanaishi na virusi vya Ukimwi  na kufanikiwa kuyafikia malengo ya 90 zote Tatu kwa mujibu wa vigezo vya Kimataifa.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema pamoja na mafanikio hayo lakini bado Ugonjwa huo ni tishio kwa Taifa na Kimataifa. Hivyo jitihada zinawajibika kuchukuliwa kupambana na mambo yanayozorotesha kasi ya Serikali katika kupambana na janga hilo thakili.

Alisema uelewa finyu usioridhisha wa baadhi ya Wanajamii juu ya Virusi vya Ukimwi  umekuwa tatizo la kuenea kwa unyanyapaa ndani ya familia dhidi ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.

Mheshimiwa Hemed alieleza tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 30.5% ya Wazanzibari {26.4% Unguja na 43.5% Pemba} wana tabia ya Unyanyapaa, tabia inayostahiki kupigwa vita  kwa nguvu zote ili lengo la kuondoa  kabisa Unyanyapaa kwa wanaoishi na Virusi hivyo lifikie asilimia sufuri { 0%}.

Akimkaribisha Mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Sena , Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi Dr. Khalid Salum Mohamed alisema Wizara imekusudia kuandaa Bajeti kwenye Mpango wake wa mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi.

Dr. Khalid alisema katika Mpango huo ambao tayari umeshapata Baraka za Rais wa Zanzibar wakati akiwahuubia Mawaziri wakati alipowaapisha utafanyiwa kwa kuwashirikisha Wadau wa Maendeleo wa ndani na Nje ya Nchi ili kpunguza changamoto zilizojichomoza ikiwemo Bajeti wakati wa utekelezaji wa Kazi hiyo.

Alizipongeza Jumuiya na Taasisi za Kimataifa chini ya mwamvuli wa Shirika la Mpango  la Umoja wa Mataifa linalosimamia mapambano dhidi ya kuondoa  kuenea kwa Virusi vya Ukimwi { UN AIDS} kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika mapambano yake dhidi ya janga la Ukimwi.

Dr. Khalid alisema jitihada kubwa zilizochukuliwa kati ya Tume ya Ukimwi Zanzibar kwa kushirikiana na Jumuiya ya kupambana na Virusi vya Ukimwi Zanzibar ZAPHA + zimeiwezesha Zanzibar kufanikiwa kupunguza maambukizi  ya Virusi na kuzifikia  zaidi ya asilimia 90 Tatu zilizokusudiwa Kimataifa.

Mapema akisoma Risala Mwakilishi wa Jumuiya kupambana na Ukimwi Zanzibar ZAPHA+ Kijana Suhaila Msham alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo hapa Nchini.

Suhaila Msham alisema Vijana wanaoishi na Virusi cha Ukimwi wamekuwa wakipata fursa za kueleza changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kawaida hasa lile na Unyanyapaa ambalo limepungua kwa kiasi kikubwa  na kuleta faraja kwao na Familia.

Aliishauri Serikali pamoja na Washirika wa Maendeleo kuanzisha Mfuko wa Ukimwi utakaowezesha kuwasaidia Walengwa pamoja na Trasmita kwa aliji ya Kituo chao cha Redio kinachotoa Elimu kwa Jamii ya namna ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Akitoa Taarifa ya Ukimwi Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ukimwi Zanzibar Dr. Salhia Ali Muhsin alisema kumekuwa na ushiriki mkubwa wa Taasisi za Serikali katika kuendeleza Programu za Ukimwi kwa Watendaji wao ambazo zimejumuisha Semina, Makongamano na hata midahalo.

Dr. Salhia alisema Elimu iliyoendezwa kwenye Programu hiyo imewezesha kupunguza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ikiwa chini kutokana na utafiti uliofanywa unaobainisha kwamba ipo silimia 12% ya wanawake wanaouza Miili yao, silimia 10% kwa Vijana wanaojihusisha na Dawa za Kulevya na asilimia 5% kwa Vijana wanajihusisha na Mapenzi ya Jinsia Moja.

Alisema Tume ya Ukimwi imefungua Vituo 174 katika maeneo mbali ya Unguja na  Pemba vya kupima damu kwa ajili ya uchunguzi wa Virusi vya Ukimwi na tayari watu wapatao Laki 170,924 wamechunguzwa Damu zao.

Alieleza kwamba hadi Mwezi Septemba Mwaka huu wa 2020 jumla ya Watu elfu 6,889 waliopata maambukizi ya Virusi hivyo wamejiunga na kuanza kupata huduma za Dawa za kupunguza makali ya Virusi.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Tume ya Ukimwi alibainisha kwamba  akina Mama wajawazito wanaokwenda kupima Afya hulazimika kufanyiwa uchunguzi wa Virusi vya Ukimwi ambapo elfu 41,976 waliofanyiwa vipimo ni wajawazito 283 wamebainika kuambukizwa virusi hivyo ikiwa ni sasa na asilimia 0.7%.

Akitoa salamu za Familia ya Mashirikia ya Umoja wa Mataifa hapa Nchini Mwakilishi wa Shirika la Mpango unaosimamia kupiga vita mapambano dhidi ya kuondoa Ukimwi Duniani { UN AIDS} Bwana George Loe alisema kazi kubwa inayotekelezwa na SMZ kwa kushirikiana na Taasisi na Jumuiya tofauti imeleta faraja kwa Umoja wa Mataifa kupitia UN AIDS.

Bwana George alisema inapendeza kuona Visiwa vya Zanzibar ni miongoni mwa Nchi chache Barani Afrika zenye maambukizi hafifu ya Virusi vipya  Ukimwi yakiwa chini ya asilimia Moja.

Alisema Shirika la Mpango unaosimamia kupiga vita mapambano dhidi ya kuondoa Ukimwi Duniani { UN AIDS} litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  katika safari yake ya kuondoa Virusi vya Ukimwi ifikapo Mwaka 2030 kwa kutumia uimarishaji wa mifumo ya Afya pamoja na kuheshimiwa Haki za Wanawake na Watoto.

Mwakilishi huyo wa Shirika la Mpango unaosimamia kupiga vita mapambano dhidi ya kuondoa Ukimwi Duniani { UN AIDS} aliishauri Zanzibar lazima iwe tayari wakati wote kupambana na Majanga ya aina yoyote pale yanapoibuka au kuleta athari katika Jamii.

Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Dunia ifikapo Tarehe Mosi Disemba ya Kila Mwaka imepangwa Rasmi kuwa ukumbusho kwa Mataifa Wanachama wa Umoja wa Mataifa juu ya Azimio la kuwa na Jamii iliyo salama na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi {VVU}.

Ujumbe wa Mwaka huu wa Siku ya Ukimwi Duniani unaeleza:- TUSHIKAMANE NA TUWAJIBIKE KUMALIZA UKIMWI DUNIANI. Ujumbe huo ukitoa wito kwa Mataifa yote Duniani kuungana katika kumaliza janga la Ukimwi.