SHIRIKA lisilo la kiserikali Zanzibar SOS limekabidhi mifuko 623 ya saruji na bati 100 zikiwa na thamani ya Zaidi ya shilingi Milioni 11, kwa Familia 38 Zilizomo katika mpango wa kuimarisha familia unaosimamiwa na shirika hilo.
Akikabidhi msada huo kwa familia hizo huko Tumbe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mjumbe wa bodi ya Shirika la SOS Zanzibar Dk.Issa Seif Salim alisema lengo la kukabidhi msaada huo ni kuwalinda watoto na kuishi katika mazingira mazuri.
Alisema familia zinapokuwa katika mazingira mazuri ya makaazi, basi hata watoto nao wataishi katika mazingira mazuri na kupata muda mzuri wa kusoma masomo yao.
Aidha amjumbe huyo wa bodi alisema SOS ipo mstari wa mbele katika kuwalinda na kuwapa maisha bora watoto, ili kufikia malengo hayo shirika limeona kwanza kuimarisha familia zao.
“Shehia ya Tumbe imekua na bahati kubwa kwetu, tumekuwa mastari wa mbele kuwasaili wananchi wa Tumbe, kupitia mradi wetu wa kuimarisha famili na tayari familia zimeweza kuimarika”alisema.
Aidh alisema kupitia mradi huo hata watoto wamehamasika kurudi skuli kuendelea na masomo yao, wakati tunaanza mradi katika shehia hii utoro ulikuwa mwingi sana.
Naye mratib wa shirika la SOS Pemba Ghalib Abdalla Hamad, alisema kuna malengo mbali mbali wamejiwekea kupitia mradi wa kuimarisha familia 2019/2022, iki ni kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, haki zao za msingi, wanapata mahitaji yao licha ya baadhi ya wakati kukumbana na changamoto ikiwemo kuzikosa haki hizo.
Alisema Pemba kunamiradi mingi ikiwa na lengo la kuinua familia, kupitia mlezi wa familia na kufikia kuwa na vikundi 10 vya kuweka na kukopo, miradi ya elimu kuhakikisha watoto wa msingi na sekondari wanapata haki zao za elimu vizuri, pamoja na kusaidia kambi za wanafunzi maskulini.
Hata hivyo aliwataka wanafamilia watakaokabidhiwa vifaa vya ujenzi, kuhakikisha msaada huo wanautumia ipasavyo kwa lengo la kuwapatia makaazi bora watoto wao.
“SOS imekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wananchi wa Tumbe, kupitia mradi wetu huu wa kuimarisha familia wananchi wameweza kunufaika na mambo mengi”alisema.
Mwenyekiti wa jumuiya ya maendeleo Tumbe Nassora Suleiman Nassor, alisema msaada huo wameupokea kwa furaha kubwa na wananchi wenyewe wamefarajika kupata msada huo.
Aliwataka wanafamilia wanaopatiwa msaada huo kuutumia kwa lengo lililokusudiwa, ikiwemo kujenga makaazi yao ili watoto waweze kuishi kwa hali nzuri.
Naye mmoja wa wanufaika wa mradi wa kuimarisha Familia Tumbe fatma Ali Hamad alisema msaada huo atautumia kwa kuendelea kujenga nyumba yake katika sehemu ambayo haijamaliza.