RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Rais Dk Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Theobald Sabi akiwa amefuatana na Meneja Uhusiano William Kallaghe na Ramadhan Lesso ambaye ni Meneja wa Tawi la NBC Zanzibar.
Katika maelezo yake Rais Dk. Hussein Mwinyi aliueleza uongozi huo kwamba amefarajika kwa kiasi kikubwa na utayari wa Benki hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali na kusisitiza kwamba mashirikiano ya hali ya juu watayapata kwani lengo ni kuwahudumia wananchi.
Alisema kuwa hatua hiyoitasaidia katika kuendeleza yale yote ambayo walielezwa wananchi wakati wa kampeni ili kuweza kuyafanyia kazi na kuhakikisha wananchi hao wanapata faraja katika kutimiziwa ahadi zilizoahidiwa.
Aliongeza kwamba hivi sasa Serikali imo katika kutayarisha maeneo ya ndani na nje na baadae kuyapambanua yale ya kushirikiana na sekta binafsi na yale ya kushirikiana na sekta ya umma.
Rais Dk. Hussein alisema kuwa msaada huo wa gari maalum ya kuchukulia wagonjwa utasaidia hasa kwa akina mama na watoto katika kuhakikisha juhudi za kupambana na vifo vya akina mama na watoto zinafanikiwa na kupatiwa ufumbuzi wa uhakika.
Aidha, aliipongeza azma ya Benki hiyo ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya afya.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Hussein alitoa angalizo kwa uongozi huo kwamba ni vyema pale wanapotaka kutoa misaada yao wakakutana na wataalamu wa sekta wanayotaka kuiunga mkono ili iwe rahisi katika kufikia malengo waliyoyakusudia.
Alisema kuwa Serikali iko tayari katika kushirikiana na Benki hiyo katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya afya, elimu na nyenginezo.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Hussein alitoa shukurani kwa pongezi zilizotolewa na Benki hiyo pamoja na Bodi na wafanyakazi wake za kumtakia kila la kheri kufuatia ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara Theobald Sabi alimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa niaba ya benki hiyo, Bodi ya Wakurugenzi pamoja na wafanyakazi wake kwa kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita na kumuahidi kuMpa ushirikiano katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2020-2025.
Aidha, Mkurugenzi huyo alimueleza Rais Dk. Mwinyi historia ya Benki hiyo ambayo imeanza rasmi mnamo mwaka 1967 na kwa upande wa Zanzibar shughuli zake zilianza rasmi mnamo mwaka 1969 huku akieleza kwamba imekuwa ikipata mashirikiano mazuri kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea ilipoanzishwa Benki hiyo.
Alieleza kuwa Benki hiyo ilitoa hisa kwa Benki ya Afrika Kusini “Absa Group Limited” kwa asilimia 55, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 30 ya hisa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kama mwanachama wa Benki ya dunia ilipata asilimia 15.
Uongozi huo ulieleza kuwa uko tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa azma ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Aliongeza kuwa Benki hiyo iko tayari kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuanza kutoa mchango wake kwa kuipa Wizara ya Afya gari la kubebea wagonjwa pamoja na kuchangia dawa za binaadamu.
Alieleza kwamba ni utaratibu uliowekwa na Benki hiyo ya NBC kutoa huduma za afya kwa kupitia gari kusaidia jamii kwa kuwasaidia wagonjwa kuwapeleka hospitali katika mikoa mbali mbali hapa Tanzania jambo ambalo wameona haja ya kutoa huduma hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Alisema kuwa miongoni mwa kazi ya benki hiyo ni kutoa huduma za kliniki za biashara kwawafanyabiashara wakubwa na wale wa kati kupitia ushirikiano huo kati ya ubia wa benki hiyo na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kutoa huduma mbali mbali za ukusanyaji fedha na huduma nyingine za kibenki kwa wateja wake pamoja na utoaji wa mikopo na mafunzokwa wajasiriamali sambamba na kutoa elimu ya kibenki.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk