
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Jamal Kassim Ali, amemuagiza Mkandarasi kutoka kampuni ya ADVENT Construction Limited wa mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za ZRB Gombani, kuhakikisha anaongeza wafanyakazi pamoja na kufanya kazi usiku na mchana, ili liweze kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Jamali alitoa agizo hilo baada ya kutembelea ujenzi wa mradi huo wa ujenzi wa ofisi za ZRB Gombani Wilaya ya Chake chake, na kusikiliza maendeleo yake akiwa katika ziara yake ya siku mbili ya kutembelea miradi na taasisi mbali mbali zilizomo ndani ya wizara hiyo.
Alisema Mkandarasi huyo anapaswa kuajiri wafanyakazi kutoka kisiwa cha Pemba, kwa ajili ya upakaji wa rangi na matengenezo ya mwisho, ili kati kati ya mwezi huu atakapokuja tena kukagua kazi hizo zimeshakamilika.
Alisema haiwezekani kuona masuala madogo madogo ikiwemo ya upakaji warangi, pamoja na matengenezo ya mwisho yanakwama kutokana na idadi ya wafanyakazi kuwa kidogo, ilhali Pemba wapo vijana wazuri wanaoweza kufanya kazi hizo.
“Zipo baadhi ya kazi zinaweza kufanywa usiku na zipo kazi zinaweza kufanywa mchana, vizuri kuwa na wafanyakazi wakutosha ila inaonekana hapa pana uhaba wa wafanyakazi”alisema.
Aidha Waziri Jamali alimtaka kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar ZRB, kuhakikisha kunakuwa na mtu mmoja kila siku anapita asubuhi na usiku katika jengo hilo, ili kuona hali ya ujenzi unavyoendelea.
Alisema hatua hiyo itapeleka jengo hilo kumalizika kwa wakati muwafaka, Corona na mvua zisiwe changamoto za kuzoretesha ujenzi huo, kwendana na kinyume na mikataba ya ujenzi.
Akizungumza na uongozi wa BPZ na Islamik Bank, Waziri huyo wa Fedha alishauri huduma za Islamik Bank kutolewa chini na sio kuwapandisha wazee kufuata huduma chini.
“Benk zozote zinazotoa huduma basi zinakuwa chini, suala la kuwapandisha juu wazee ni tatizo, hili suala linapaswa kuangaliwa kwa kina”alisema.
Aidha aliutaka uongozi wa PBZ kuendelea kuwaelimisha wananchi, kwa kutumia magari ya matangazo ili kuelezea huduma mbali mbali zinazotolea na bank hiyo.
Kwa upande wa ujenzi wa Ofisi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF Tibirinzi, Waziri huyo wa Fedha Zanzibar aliupongeza mfuko huo kwa hatua kubwa walioichukua, pamoja na kuridhika na ujenzi wake ambao kwa sasa umeshafikia asilimia 90%.
Naye Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar Josef Abdalla Meza, alisema atasimamia maagizo yote yaliyotolewa na Waziri huyo, yanafuatwa kwa vitendo ili kuhakikisha jengo hilo linamalizika na linafunguliwa katika sherehe za Mapinduzi.
Alisema ndani ya Mwezi wa Disemba jengo litakuwa limeshakamilika, kwani vifaa vyote tayari vimeshafika Zanzibar ilichobakia ni kuwasilishwa katika eneo la ujenzi.
Naye Mkandarasi kutoka kampuni ya Advent Consternation Frank Mohan, alisema changamoto kubwa iliyopelekea kutokumalizka kwa wakati ni kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikishenya, pamoja na kuchelewa kufika kwa baadhi ya vifaa kutoka nje ya nchi, ila kwa sasa meli imeshawasili Zanzibar kilichobakia ni kusubiri kuteremsha vifaa hivyo.
Akitika ziara hiyo waziri Jamali alitembelea ofisi za wizara yake Gombani, Benki ya Watu wa Zanzibar tawi la Chake Chake, Shirika la Bima na Mradi wa ofisi mpaya za ZSSF Tirinzi na kituo cha mafuta cha GAPCO Wesha.