NA SAID ABRAHMAN.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya ya Wete, kimewataka watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa juhudi na kutimiza wajibu wao.
Akifungua kikao Cha halmashauri ya CCM Wilaya ya Wete, kilicho jumuisha watendaji wa sekta mbali mbali za Serikali, kimefanyika huko katika ukumbi wa jamhuri hall Wete.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Wete Kombo Hamad Yussuf, alisema chama hicho wakati wa kampeni kiliahidi kufanya kazi, ili kiweze kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Alisema kuwa uchaguzi umekwisha sasa kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi imeanza, hivyo jukumu kubwa lililopo mbele yao ni kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza yale yote ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.
Aidha Mwenyekiti huyo aliwapongeza wanachama Cha Mapinduzi na wananchi, kwa kukichagua Chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita na kukiletea ushindi wa kishindo na hatimae kuunda Serikali.
“Uchanguzi umekwisha na CCM imeshinda, jambo kubwa ambalo lipo mbele yetu ni kufanya kazi kwa bidii, kuweza kuwapelekea wananchi wetu maendeleo,”alisema.
Hata hivyo aliwataka kuwambua kuwa bado wanapengo kubwa katika jimbo la Pandani, ambalo mwakilishi wake alifariki dunia hivyo aliwashauri wanaccm kujindaa kuhakikisha jimbo hilo linaingia katika mikono yao.
Mapema akimkaribisha Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Wete, Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo Salim Khamis Haji, aliwataka viongozi hao kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili waweze kuwatumikia wananchi wao.
Aidha alisema endapo viongozi watabadilika, maendeleo makubwa yanaweza kupatikana katika nyanja zote, kwani serikali ya nane (8) imepania kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa ni kitovu Cha maendeleo.
“Tuhakikishe kila mmoja wetu anatimiza wajibu wake, sio muda huu tena wakusukumana, wamekuwa na imani kubwa na uongozi uliopo madarakani,alifahamisha.
Hata hivyo alisema kuna baadhi ya wafanyakazi, wanazifanya ofisi zao kama sehemu ya kwenda kubadilishana mawazo, wengi wao ikifika saa nne za asubuhi 4:00 wanaanza safari ya kurudi majumbani kwao au wengine masokoni na madukani, jambo ambalo halikubaliki kwa mtumishi wa umma.
Akizungumza suala zima uanzishwaji wa miradi, Katibu Salim alieleza kuwa miradi mingi imeanzishwa lakini kutokana na usimamizi usio kuwa mzuri, miradi hiyo imedumaa na haileti tija kwa wananchi.
Hata hivyo aliwataka watendaji hao kubuni vyanzo vipya vya mapato, ambavyo vitaweza kuleta maendeleo katika Wilaya yao, pamoja na kubuni nyengine mbadala ambazo zitaweza kuwaingizia mapato.
Mkurugenzi wa Baraza la mji Salim Juma Pandu, aliwakaribisha viongozi wa CCM katika Ofisi yake na kuwataka kuwa karibu na Ofisi hiyo, pamoja na kuupongeza uongozi wa chama hicho huku akiwataka kuendelea kutoa mashirikiano kwa taasisi zote zilizomondani ya wilaya hiyo.