Thursday, October 31

Milioni 1.6 yakabidhiwa kwa uongozi wa Masjid Aisha Furaha Mbuyuni kwa ajili ya ujenzi wa hodhi.

MWAKILISHI wa Jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar katikati na Mbunge wa Jimbo la Wawi Khamis Kassim Ali wa kwanza kushoto, wakimkabidhi mzee wa masjid Aisha Furaha Mbuyuni Mohamed Massoud Said wa kwanza kulia shilingi Milioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa hodhi la kuhifadhia maji katika mskiti huo. .(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

MBUNGE na Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Kisiwani Pemba, wameukabidhi uongozi wa Masjid Aisha Furaha Mbuyuni shilingi Milioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa hodhi la kuhifadhia maji mskitini hapo.

Hafla hiyo ya makabidhiano ya fedha hizo, zimefanyika ndani ya msikiti huo ikiwa ni miongoni mwa ahadi walizozitoa viongozi hao wa jimbo hilo kwa wananchi wakati wakiomba kura.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, mwakilishi wa jimbo hilo Bakar Hamad Bakar, alisema wamelazimika kurudisha ihsani kwa uongozi wa msiki huo, kutokana na kuwaamini kuwa viongozi wao wa jimbo.

Alisema katika kipindi hiki ambacho wananchi wa mbuyuni Furaha waliwaamini, basi watahakikisha wanajenga madrasa mbili za kisasa ili kuwapa nafasi watoto kusoma katika mazingira mazuri.

“Kwa sasa viongozi wetu na wazee tunaomba mutupokelee hiki tulichojaaliwa nacho, ili kutimiza lile lengo la msikiti wetu”alisema.

Hata hivyo aliwataka wanakamati hao kutambua kuwa sasa siasa zimepita kilichobakia ni kuhimizana katika suala la maendeleo, kwani viongozi hao ni wa jimbo zima na wapo tayari kuwatumikia wananchi wote katika suala la maendeleo.

Naye mbunge wa jimbo hilo Khamis Kassim Ali, aliwashukuru wananchi wa Mbuyuni Furaha kwa kuendelea kuwaamini, huku akiwataka kuhakikisha wanakuwa mstari wambele katika suala la maendeleo.

Akitoa shukurani kwa niaba ya uongozi wa msikiti huo, shekhe Khamis Said Massoud, aliwashukuru viongozi hao wa jimbo kwa masaada walioutoa, kwani umefika katika wakati muwafaka wa kulijenga hodhi lao la kuhifadhia maji.

Aidha aliahidi fedha hizo kutumika kwa lengo lililokusudiwa la kujengwa hodhia kuhifadhia maji na sio jambo jengine, huku akiwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu juu ya msaad walioutoa.

MWAKILISHI wa Jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar wa mbele akiwa amefuatana na Mbunge wa Jimbo hilo Khamis Kassim Ali, wakikagua hodhi la kuhifadhia maji katika Masjid Aisha Furaha Mbuyuni, ambapo walikabidhi Milioni 1.6 kwa uongozi wa msjid Aisha kwa ajili ya kujenga hodhi jengine.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)