RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amewataka viongozi wa vyama vya michezo Zanzibar kusimamia michezo kwa uweledi ili kurudisha hadhi ya michezo ambayo imepotea Zanzibar.
Dkt. Mwinyi alisema tayari alishamuagiza waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, kukaa na wadau wa michezo na ili kuondosha tafauti zao kwa lengo la kuendeleza michezo nchini.
Kauli hiyo aliitoka katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Fidel Castro, wakati alipokua akizungumza na makundi mbali mbali ya wajasiriamali wakiwemo wanamichezo, ikiwa ni ziara yake ya siku mbili Kisiwani Pemba.
Alisema lazima uongozi wa vyama vya michezo ujipange, kwani paemba walifika hadi kutaka ligi ichezwe kwao na Unguja kwao, baadae timu zikutane na kutafuta bingwa kutokana na kutokua na uwezo wakusafirisha timu.
“Mimi najua chama cha mpira wa miguu ZFF kinamatatizo lazima tuweke wazi, tusipojipanga matatizo yataendelea, kwa sababu tumeshapata wa kudhamini wapo tayari kudhamini michezo, kwa sababu tumeshajua kuna utaratibu wa kujenga viwanja na kuinua vipaji, tunahitaji kujipanga katika vyama vyetu vya michezo, ili viongozi wasije wakawa tatizo la kuendeleza michezo Zanzibar”alisema.
Aidha Dk Mwinyi alisema alikutana na wanamichezo wakati akiomba kura katika ukumbi huo huo, huku wakimtaka kuipakipaombele michezo na tayari ameshakutana na wadau wa michezo na wameshakubalina kudhamini michezo Zanzibar.
“Tumekubaliana kwamba wakati umefika sasa kuwe na udhamini katika michezo au ufadhili, haiwezekani ikapangwa michezo bila ya fedha, michezo inahitaji fedha watu wanatakiwa kusafiri kwenda huku na kule, watu wanahitaji vifaa bila ya udhamini michezo haitokwenda mbele,”alisema.
Hata hivyo alifahamisha kuwa wafanyabiashara aliokutana nao, wameahidi kuwa tayari kusaidia na kuhakikisha wanaiendeleza michezo ya hapa Zanzibar.
Naye mdau wa michezo Pemba Issa Kassim Juma, ambe ni kocha wa leseni C, alimpongeza Dkt.Mwinyi kwa hutuba yake na msimamo wake katika sekta ya michezo, huku akiwataka viongozi wa ZFF ambao hawawezi kwenda na kasi ya Rais vizuri kupumzika.
Alisema viongozi waliopo hawaendeni na kasi ya Rais kulingana na malengo yake, vizuri kukaa pembeni mapema kabla ya kuja kuondolewa ili kupisha wadau wenye uwezo wakuliendesha soka la Zanzibar.
Katibu wa Timu ya Chipkizi Adam Abdalla, alisema hutuba ya rais imewapa matumaini makubwa na kuhakikisha soka za Zanzibar litaendelea mbele, licha ya changamoto zilizopo zaviongozi wa mpira nchini.