Thursday, October 31

KAIMU Mkurugenzi wa Baraza la mji Mkoani awapongeza wananchi wa Shehia ya Mkungu..

 

NA SAID ABRAHMAN.

 

KAIMU Mkurugenzi wa Baraza la mji Mkoani Dk, Mohammed Faki Saleh amewapongeza wananchi wa Shehia ya Mkungu Wilaya ya Mkoani kutokana na kubaini changamoto zinazozikabili katika Shehia yao.

 

Alisema kuwa kazi hiyo ya kufichua changamoto, haikuwa rahisi kwani kutokana na muda ambao umepangwa kuwasilisha changamoto hizo.

 

Dk, Mohammed aliyasema hayo huko Mkungu wakati alipokuwa akizungumza na wananchi katika ufungaji wa mpango shirikishi wa maendeleo, ulioandaliwa na taasisi ya Zanzibar Millelle Foundation.

 

Dk, Mohammed aliwataka wananchi wa Shehia hiyo kushirikiana na kamati yao, ili kuhakikisha yale yote ambayo yameibuliwa yanafanyiwa kazi.

 

Aidha Dk, Mohammed aliwafahamisha wananchi hao, kuwa kile ambacho kimeibuliwa na kamati hiyo waone ni Cha kwao na kina wahusu wao, hivyo ni wajibu wao kukaa pamoja na kuyaunga mkono.

 

Hata hivyo aliipongeza taasisi ya Millelle Foundation, kwa kuweza kuandaa mpango huo na kushirikisha jamii katika kubuni zile changamoto zao zilizomo katika Shehia zao.

 

Nae Mkurugenzi wa Zanzibar Millelle Foundation Abdalla Said Abdalla aliwasisitiza wanajamii ya Mkungu, kushirikiana pamoja na kamati yao ili kuhakikisha yale yote ambayo yameibuliwa kuwa na changamoto zao zinafanyiwa kazi.

 

Aidha alifahamisha kuwa taasisi ya Millelle Foundation ni taasisi ya isiyo ya kiserikali, ambayo madhumuni yake ni kuwasaidia wananchi katika kuwatatulia matatizo yao.

 

Alisema kuwa taasisi yao ipo kisheria na iko huru na imepewa kibali Cha kufanya kazi ndani ya Visiwa vya unguja na Pemba, kwa lengo kuwaletea wananchi maendeleo.

 

“Taasisi ya Millelle Foundation ni taasisi huru na imepewa kibali na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya kazi zake ndani ya Visiwa vya Zanzibar ili kuwaletea maendeleo wananchi wake” alisema Abdalla.

 

Alisema Milele inashughulikia zaidi masuala ya kijamii ikiwa ni pamoja na elimu, afya na hata ujengaji wa barabara za vijijini, kusaidia wanafunzi ambao wanapata nafasi ya kuelendelea masomo yao, ambao wanafanya vizuri katika mitihani yao huku akitoa ahadi kuwa wale wote ambao watapasi michepuo milele itawasaidia.

 

Nao wananchi hao walibainisha kuwa changamoto kubwa ambazo zinawakabili, katika Shehia yao ni pamoja na sekta ya kilimo, afya na barabara.

Akiwasilisha changamoto ya kilimo, Omar Khamis aliwataka wanajamii hao kutumia fursa zilizopo (ardhi,mabonde na maji) ili kujiongezea kipato Chao, kwani mpango mkakati wa kilimo wamejipanga kutoa taaluma kwa wananchi wao kuhusiana na kilimo Cha kisasa.

 

“Katika mpango shirikishi wa kilimo,tumeona tuwape elimu wananchi wetu juu ya kulima kilimo kilicho bora ili waweze kupata mazao yaliyo Bora, lakini pia tutafungua darasa kwa vijana ili tuweze kuwasomesha namna ya ulimaji Bora,” alifahamisha Omar.

 

Nae Fatma Ali alieleza mpango mkakati wa elimu, wamepanga kujenga uzio katika Skuli ya Mahuduthi ili kudhibiti uharibifu katika Skuli hiyo.

 

Kwa upande wake Khamis Mohammed alisema mpango wa afya ni kujenga kituo Cha afya ili kupunguza masafa kutafuta huduma hiyo katika kituo Cha Kengeja, kwani jamii imekaa na kuona ni vyema kuwa na kituo chetu Cha afya ambacho kitaweza kutoa huduma kwa wananchi wa Shehia hii na Shehia nyengine.

 

Mpango shirikishi wa maendeleo wa Shehia umendaliwa na taasisi ya Millelle Foundation ambapo katika Shehia hiyo muda wa siku sita (6) wananchi wa Mkungu walikaa pamoja na kuibua changamoto zao katika Shehia yao.