Thursday, October 31

Mbunge na Mwakilishi Wawi wakabidhi maskani ya wazee

 

 

 

 

 

 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mwalim Kiombo Hassan Juma, akimkabidhi seti ya TV mwakilishi wa wazee wa maskani ya Wazee Machomanne Khamis Iddi Songoro, TV hiyo imetolewa na viongozi wa Jimbo la Wawi Mbunge na Mwakilishi

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mwalim Kiombo Hassan Juma, amewataka Wananchi kuiunga mkono serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliyo chini ya umoja wa kitaifa kwa kuipa mashirikiano ili kuona malengo ya hatua za maendeleo yanafikiwa kwa kasi.

Alisema serikali hiyo inayoongozwa na Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi, tayari imeshaanza kupanga safu za viongozi wake, huku ikiwa na dhamira ya kuwapatia wananchi maendeleo bora.

Mjumbe wa kamati Kuu ya CCM Taifa aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akikabidhi maskani ya wazee Machomanne, kwa uongozi wa maskani hiyo baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa na Mbunge na mwakilishi wa jimbo la Wawi.

Alisema shuhuli za uchaguzi zimemalizika na serikali ya Umoja wa kitaifa inayowahusisha wazanzibari wote, hivyo aliwataka kushirikiana katika kuunga mkono serikali hiyo.

“Serikali ya umoja wa kitaifa haina maana aliyemo humo, kuchukua juhudi zaidi kujiimarisha zaidi katika chama chake au katika itikadi zake, lengo ni kuwatumikia wananchi wa Zanzibar”alisema.

Alifahamisha kuwa katika suala la kuendeleza nchi, hakuna haja ya kuendeleza mifarakano badala yake kuwa kitu kimoja, katika kujenga nchi na kuwa kama nchi nyengine duniani zilizopiga hatua kimaendeleo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar, alisema jimbo hilo linakabiliwa na changamo kadhaa ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama, Michezo, skuli, barabara na akinamama wenye vikundi vya ushirika na vijana na bado wanakabiliwa ukosefu wa mitaji ya kuendeleza vikundi vyao.

“Tayari baadhi ya maeneo tumeshaanza kutatua changamoto za wananchi ikiwemo maji huko Mgogoni na kuahidi tatizo la maji kuwa historia, pamoja na baadhi ya ameneo mengine katika jimbo letu ikiwemo Gombani”alisdema.

Naye Mbunge wa jimbo la Wawi Khamis Kassim Ali, aliwataka wananchi wajimbo la Wawi kuwapatia mashirikiano katika suala zima la kuleta maendeleo ndani ya jimbo hilo, kwani Serikali ya awamu ya nane pamoja na wabunge na wawakilishi wamedhamiria kupelekea maendeleo katika jimbo hilo.

Akizungumza kwa aniaba ya wazee wa maskani ya Wara na Mkoroshoni, Mzee Khamis Iddi Songoro alisema kwa Pemba bado maskani hiyo ya wazee ndio inayoongoza kudumu kwa muda mrefu.

Alisema kwa sasa wazee wenzao saba tayari wameshatangulia mbele ya Haki, hivyo itaendelea kuwa chemchemu ya kuvuna vijana kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita na kuiweka tena CCM madarakani.

Akisoma risala ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi Maskani ya Wazee Machomanne Mwanachama wa CCM Asha Ame Mshenga, alisema maskani hiyo ilianzishwa na Marehemu Dk.Omar Ali Juma kwa lengo la kuwaunganisha wanaCCM wote, ili kupata sehemu sahihi ya kupanga mipango ya chama pamoja na kuongeza juhudi zakuongeza wanachama wapya.

“Maskani ni chachu ya mafanikio ya chama cha Mapinduzi, pia ni sehemu ya kujenga madarasa ya Itikadi ya chama, ndio chimbuko la msingi la maazimio ya kuimarisha chama”alisema.

Aidha alisema maboresho ya maskani hiyo ya wara ilikuwa ni kilio cha muda mrefu cha wanachama wa jimbo hilo, ambapo ukarabati huo hadi kukamilika kwake umegharimu zaidi ya shilingi Milioni tano (5,000,000/=).