ZAIDI ya wananchi 50 wa kikundi cha Nguvu Hazichezewi cha Mvumoni wilaya ya Chake Chake, kinachojishughulisha na uzalishaji wa chumvi wanatarajiwa kuondokana na umaskini wa kipato, baada ya kupokea msaada wa vifaa vya kuzalisha zao hilo.
Vifaa hivyo vilivyotolewa na muakilishi wa jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar na mbunge Khamis Kassim Ali ni pamoja na majanareta mawili, bero tatu, shoka, mipira, pauro, mapanga na mashine ya kuvutia maji, vitu vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 3.1 pamoja na kukabidhi shilingi laki mbili keshi (200,000/=)kwa kikundi hicho.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa katika kijiji cha Mvumoni mshikafedha Sharifa Khamis Ali, alisema wanatarajia kuongeza uzalishaji wa chumvi, baada ya kupata vifaa hivyo kwani ni kilio cha muda mrefu ambao ukisababisha uzalishaji kuwa mdogo.
Alisema muda mrefu wakifanya shughuli za uzalishaji wa chumvi kwa kubahatisha, hali ambayo ikiwakatisha moyo lakini kwa sasa nema imeshuka kwao.
“Sasa kila mmoja wetu hapa amekua na furaha viongozi wetu wametuahidi ndani ya siku tatu leo wametimiza na kila mmtu anaona kilichofanyika”alisema.
Aidha wanachama wa Nguvu Hazichezewi waliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na viongozi wao wa jimbo la Wawi, kwa kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo muakilishi wa jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar, amewataka wananchama hao kufanya kazi kwa ajili ya uzalishaji, ili kukuza uchumi wao na serikali kwa ujumla.
Alisema katika kuzalisha kwao wanapaswa kutambua umuhimu wa kuvitunza na kuvithamini vifaa hivyo, ili viweze kudumu kwa muda marefu sambamba na kuachana na matumizi ya kimazowea katika vifaa hivypo.
“Hivi ni vifaa vyetu sote lazima katika hiki kikundi muhakikishe munakua makini katika kuvitunza na kuvithamini ili viweze kudumu kwa muda mrefu”alisema.
Alifahamisha kwamba jimbo la wawi linachangamoto nyingi, hivyo watajitahidi kuzitatua kidogo kidogo ili kufikia malengo ya jimbo hilo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya chake chake Khamis Salum Khamis, alitanabahisha wanachama hao kupokea kwa vifaa hivyo isiwe chanzo cha migogoro baina yenu,na badala yake iwe na chachu ya maendeleo kwani ndio ajira zao.
Akiwasalimia wanachama hao mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir amesema serikali ya awamu ya nane inakwenda na kasi ya maendeleo yanayojali makundi tofauti katika mabadiliko ya kiuchumi katika Nyanja mbali mbali.