Friday, November 1

RC Kaskazini asifu juhudi za mbunge kusaidia jamii

Mbunge wa Viti maalumu Wawake Mkoa wa Kaskazini Pemba Asya Sharif Omar akishiriki katika ujenzi wa madrasa ya Kur-an kwa kuweka jiwe na udongo, kabla ya kukabidhi msaada wa mifuko 15 ya saruji kwa uongozi wa madrasa hiyo

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, amesifu juhudi za wananchi wa Kizimbani wilaya ya Wete za kuanzisha ujenzi wa madrasa ya kur-ani, ili watoto wao wapate elimu ya dini ya kiislamu karibu na mazingira wanayoishi.

 

Alisema suala hilo ni jambo jema ambalo litawasaidia kwa kiasi kikubwa watoto kufuata elimu hiyo masafa marefu, huku akiahidi kusimamia ujenzi wa madarasa hiyo inakamilika na watoto wanaweza kusoma kwa bidii.

 

Salama alisema hayo kwenye ujenzi wa madrasa hiyo Kizimbani, wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa mifuko 15 ya saruji na shilingi laki moja na elfu hamsini za mawe (150,000/=) msaada uliotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu Wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Asia Sharif Omar.

 

Alisema kuwepo kwa madrasa hiyo itawasaidia watoto kupata  nafasi ya kujifunza mambo mbali mbali ya kiislamu, ambayo ni mustakabali bora wa maisha yao ya duniani na akhera, sambamba na kuwajenga katika maadili bora.

 

“Hili ni jambo jema na zuri ulioloanza kulifanya, hapa sio kama unasaidia ujenzi bali unajenga akhera yako fadhila nyingi zitapatikana, hii ni sawa na sadakat jaaria ambayo umeitoa leo ikizingatiwa watakaonufaika hapa ni watoto”alisema.

Alifahamisha kuwa licha ya elimu ya kur-an watoto watakaopatiwa, bali hata elimu nyengine pia watapatiwa ili wakitoka hapo wawe watoto wema mitaani.

 

Hata hivyo aliwataka wananchi na viongozi wengine kujitokeza, kuunga mkono juhudi mbali mbali zilizochukuliwa na wananchi wa kizimbani kwa kuanzisha madrasa yao.

 

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba, Asia Sharif Omar alisema ataendelea kuwapatia wananchi wa mkoa huo misaada tofauti, kulinga na mahitaji yao kwani wapo kuwasaidia wananchi katika shughuli za maendeleo.

 

Alisema baada ya wasimamizi wa madrasa hiyo kumfuata na kumuelezea mahitaji yake, ndipo alipoamua kwenda kukabidhi mifuko hiyo ili madrasa hiyo iweze kusimama.

 

Alifahamisha kuwa baada ya kusimama itaweza kuwapunguzia masafa marefu watoto kufuata elimu hiyo ya dini, mpaka wavuke barabara upande wa pilia jambo ambalo lilikuwa likiwapa tabu watoto hao.

Akitowa neno la shukrani msimamizi wa ujenzi wa madrasa hiyo, Mzee Rashid Said Khalfan alisema wazee wa eneo hilo wameamuwa kujenga madrasa hiyo, ili watoto waondokane na usumbufu wa kuifuata elimu hiyo masafa marefu.

“Eno lote la kizimbani lina madrasa mmoja tu tena iko upande wa pili, watoto wanakata barabara wanagongwa na gari hapa wapo watoto wengi wamekuwa walemavu na wengine wamefariki kwa kugongwa na gari”alisema.

 

Hata hivyo aliwaomba viongozi mbali mbali kujitokeza kwa wingi kusaidia ujenzi wa Madrasa hiyo, kwani bado inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo tufali, saruji, mchanga, bati, madirisha, milango pamoja na fedha za kulipia mafundi.