NA SAID ABRAHAMAN.
MWAKILISHI wa jimbo la Ziwani Wilaya ya Chake Chake Suleiman Makame Ali, ameipongeza taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kutokana na juhudi zake za kuwaletea wanachi wa Zanzibar maendeleo.
Alisema kuwa Milele ni taasisi moja wapo ambayo imekuwa ikifanya kazi, kubwa ya kusaidia jamii katika kuharakisha maendeleo yao.
Makame aliyasema huko katika Kijiji cha Michungwani Shehia ya Michungwani, Wilaya ya Chake Chake wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Shehia hiyo
Mwakilishi huyo aliwataka wananchi hao kushirikiana na taasisi hiyo, katika kuhakikisha yale yote ambayo wameyapanga katika mpango wao shirikishi wa Shehia, yanafanyika bila ya pingamizi yeyote.
Sambamba na hayo alieleza kuwa atahakikisha anaweka nguvu zake zote kwa Serikali, ili kuhakikisha barabara kutoka Kijangwani hadi Birikau ambayo taasisi hiyo imeahidi kuitengeza ahadi hiyo inakamilika.
“Milele ni taasisi moja wapo hapa Zanzibar ambayo inafanya kazi kubwa sana ya kupeleka maendeleo, katika sehemu mbali mbali za visiwa hivi, hivyo ahadi yao ya kutengeneza barabara kutoka Kijangwani hadi Birikau ni sawa ” alisema Mwakilishi huyo.
Hata hivyo aliwaomba wananchi wa Shehia ya Michungwani kushiriki katika mikutano ya kujadili maendeleo katika Shehia, ili waweze kutoa changamoto zao zinazowakabili katika Shehia.
Mapema Mkurugenzi wa taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Abdalla Said Abdalla, aliahidi katika mkutano huo kuitengeneza barabara ya kutoka Kijangwani hadi Birikau kwa kiwango cha lami.
Alifahamisha kuwa tayari taasisi hiyo imeshatenga zaidi ya Tsh, billioni 2 ambazo zitatumika katika ujenzi huo huku akiwataka wananchi kushirikia wakati wa ujenzi wabarabara hiyo utakapoanza.
Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi kutafuta eneo zuri, ambalo watalitumia katika kujenga Skuli ya Chekechea kwani hatoweza kutoka mtu kuwatafutia eneo hilo.
Nao wananchi hao walieleza kuwa changamoto kubwa ambao wameziona katika Shehia yao ni pamoja na tatizo la elimu, afya na kilimo bora.
Kassim Ali Bakar ambae ni miongoni mwa wana kamati ya maendeleo ya mpango shiriki katika Shehia hiyo, alieleza kuwa kwa upande sekta ya kilimo ni kupatiwa watalaam ambao wataweza kuisaidia jamii kubadilisha kilimo walichokizoea.
Aidha alifahamisha kuwa mbali na kazi hiyo lakini pia mtalaam huyo aweze kubuni mbinu mbali mbali za uzalishaji wa mazao pamoja mifugo katika Shehia hiyo.
Sambamba na hayo kupatiwa elimu kwa wananchi wa Shehia hiyo juu ya kilimo mchanganyiko kwani shamba ambalo litalimwa kilimo Cha aina moja mara nyingi huwa linashambuliwa na wadudu kuliko lile shamba ambalo litakuwa linalimwa mazo tofauti.
“Lakini kupatiwa watalaam ambao watawaelekeza wana jamii ya Michungwani katika kujikita zaidi kwenye kilimo Cha kisasa na kuepukana na kilimo walichokizoea,’ alifahamisha Kassim.
Nae Omar Ali alieleza kuwa katika sekta ya elimu changamoto kubwa katika skuli yao ya Birikau ni uhaba wa madarasa ya kusomea kwani bado wanafunzi ni wengi na hivyo inawalazimu muda mwengine baadhi yao kujisomea nje.
Nae Said Juma Said alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya afya tatizo hilo lipo kwani wanatumia masafa marefu kutafuta matibabu kwani hulazimika kutafuta huduma katika kituo Cha Gombani.
Hata hivyo aliiomba jamii kushirikiana pamoja kulitatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kutafuta msaada wa kumaliziwa jengo lao lililopo katika Kijiji cha Birikau.