MARYAM SALUM, PEMBA
Jumla ya Tshs Bil, 2,469,061,394.70 zimekusanywa na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Pemba sawa na asilimia 61, ikiwa makusanyo ya miezi 5 kuanzia July hadi Novemba 2020.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Ofisa mdhamini Idara ya Forodha Pemba, Yussuf Haji , kwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais fedha na mipango Jamal Kassim Ali kwenye ziara yake aliyoifanya hivi karibuni Kisiwani humo.
Alisema malengo ya makusanyo katika kipindi hicho ni Tshs 4,054,181,414.00 ambayo hayajafikiwa kwa sababu mbali mbali ikiwemo hofu ya wafanyabiashara kipindi cha uchaguzi mkuu.
Alieleza kuwa makusanyo ya kodi mwaka wa fedha uliopita 2019/2020 Mamlaka hiyo Pemba ilipangiwa kukusanya Tshs 7,990,155,250.50, ambapo iliweza kukusanya Tshs 7,289,195,658.58 sawa na asilimia 91.
“Kwa mwaka huu wa fedha 2020-2021 TRA kwa upande wa Pemba imepangiwa kukusanya Tshs, 10,038,754,876.51, ambapo malengo haya Idara ya forodha imepangiwa kukusanya Tshs, 3,265,242,150.00 na Idara ya kodi za ndani imepangiwa kukusanya Tshs, 6,773,512,726.51,” alieleza afisa huyo.
Alifahamisha kuwa mikakati ya TRA Pemba katika kuongeza makusanyo ya kodi kwa mwaka huu, kufuatilia taasisi za Serikali zilizokodi majengo kwa Wafanyabiashara na kuhakikisha wanalipa kodi inayostahiki.
Alieleza mkakati mwengine ni kuwasajili Wafanyabiashara wapya na kuhakikisha wote wenye madeni ya kodi wanalipa, na kufuatilia mahoteli yote yaliyopo Kisiwani humo, ambayo yanafanya biashara za hoteli bila kusajiliwa.
“Pia tunafuatilia sekta ya wakandarasi kuwaingiza katika wigo wa kodi,na kuhakikisha Wafanyabiashara wanapita katika taasisi za kodi kabla ya kupatiwa leseni za biashara na mabaraza ya miji na taasisi nyengine zinazotoa leseni ya biashara,”alieleza.
Aidha Ofisa huyo alieleza kuwa mamlaka hiyo pia imeweka mkakati wa kuimarishwa kwa ulinzi wa doria baharini na nchi kavu na kupatiwa mashirikiano ya karibu kutoka taasisi za ulinzi na vyombo vya Serikali.
“Pia mamlaka inampango wa kuishauri Serikali kuwahamasisha wawekezaji wa ndani kuwekeza katika sekta za viwanda, Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ili tuweze kukuza uchumi wa Zanzibar,”alifahamisha afisa.
Alisema pia wataishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga bandari rasmi katika eneo la Kaskazini Mashariki ya Kisiwa cha Pemba Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini.
Yussuf , alifahamisha kuwa miongoni mwa majukumu makuu ya Mamlaka ya TRA ni kukadiria kukusanya na kuhesabu mapato yote ya Serikali kuu, na kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari.
“TRA pia inapambana na vitendo vyote vya udanganyifu na ukwepaji kodi,kuboresha huduma zinazotolewa na Mamlaka kwa walipa kodi, pamoja na kuishauri Serikali masuala yote yanayohusu sera za kodi,” alisema.
Akitaja baadhi ya changamoto ambazo zinaikabili TRA Pemba ni pamoja na taasisi nyingi binafsi zenye matawi yake Pemba kulipa kodi ya zuio(Withholding Tax ) makao makuu Tanzania bara.
“ Pia kuwepo kwa biashara ya magendo inayofanyika baharini na nchi kavu imekuwa chanzo kinachopelekea kuwepo kwa punguzo kubwa juu ya mapato ya taasisi zetu za kodi, kwani wafanyabiashara wengi waliopo Kisiwani Pemba ni wadogo wadogo (SME’s),”alisema.
Hata hivyo alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Pemba ipo na Idara nne(4) na zikiwa na Wafanyakazi 13, wakiwemo wanaume 8, na wanawake 5.