KIU ya Maendeleo pamoja na upatikanaji wa huduma za msingi ya Kijamii walizonazo Wananchi wa Kijiji cha Kibumbwi mbayo ni changamoto ya muda mrefu imeonyesha njia ya kupata Muarubaini kufuatia ziara maalum ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdullla aliyoifanya kujua kero zinazowakabili Wananchi hao.
Muarubaini huo umepatikana kufuatia Wakuu wa Taasisi zinazosimamia huduma za Maji safi na salama, Umeme, Afya, Elimu pamoja na Miundombunu ya Mawasiliano ya Bara bara kuahidi mbele ya Mheshimiwa Hemedi kwamba huduma hizo zitafikishwa katika Kijiji hicho ndani ya Miezi Mitatu kuanzia sasa.
Mmoja wa Wananchi wa Kijiji hicho ambae ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Bwana Mkombe Juma Khamis alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wamepata matumaini makubwa kutokana na kasi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane jinsi inavyoendelea kujipanga katika kuwaondoshea kero Wananchi wake.
Bwana Mkombe alisema ujio wa Mheshimiwa Hemed ndani ya Kijiji hicho akiwa Kiongozi wa kwanza wa ngazi ya Juu Serikalini imeonyesha nia safi ya Serikali kutaka kuwapatia Maendeleo wanayoyalilia kila kukicha wakiona wivu kwa wenzao wa Vijiji jirani.
Naye Bibi Vatima Amour Zonge wa Kijiji hicho alisema ukosefu wa Skuli ya Msingi ndani ya Kijiji chao imekuwa changamoto kubwa zinazowakabili Watoto wao na hulazimika kufuata elimu masafa ya mbali ya Upenja na Kiwengwa.
Bibi Vatima alisema huduma za Afya nazo zimekuwa mtihani mkubwa hasa kwa Akina Mama wajawazito pale wanapofikia muda wa kujifungua wanakabiliwa na hatari kubwa wakati mwengine hutishia hata uhai wao pamoja na Watoto.
Wakitoa ufafanuzi wa changamoto hizo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Nd. Mussa Ramadhan Haji na Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar {ZECO} Nd. Hassan Ali waliwahakikishia Wananchi hao kwamba huduma hizo muhimu zitasogezwa ndani ya Kijiji hicho katika kipindi cha si Zaidi ya Siku 90.
Wakuu hao wa Taasisi zinazosimamia huduma ya Maji na Umeme walisema gharama za Miradi hiyo zitatengwa ndani ya Fedha za Taasisi zao na kuwaomba ananchi hao kuridhia ukataji wa Miti au vipando vyao kwa zile sehemu itakazopita Miundombinu ya Miradi hiyo.
Naye kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Abdullah Ali Mwinyi na kwa niaba ya Muwakishi wa Jimbo hilo Mh. Asha Abdullah wamebeba dhaman ya kuchangia Mafuta kwa ajili ya vyombo vitakavyotumika kusafisha Bara bara iendayo kwenye Kijiji hicho kwa hatua ya Awamu ya kwanza.
Akizungumza na Wananchi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alionya na kutahadharisha kwamba Kiongozi yeyote wa Taasisi hizo aliyetoa ahadi na endapo hataitekeleza kwa wakati aliosema yeye akiwa Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali hatasita kumuwajibisha mara moja.
Mh. Hemed alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane haina muda tena wa kushirikiana na mzembe wakati tayari imeshaahidi katika kipindi cha Kampeni za Uchaguzi kuwatumikia Wananchi kwa kasi kubwa ili kukidhi matarajio yao.
Alielezea Imani yake kwamba ifikapo Mwezi Aprili atalazimika kufanya ziara nyengine kujiridhisha endapo zile ahadi zilizotolewa na Wakuu wa Taasisi hizo zimetekelezwa na kuiona Kibumbwi inabadilika haraka Kimaendeleo hasa kutokana na Zaidi ya asilimia 70% ya chanagmoto zilizojitokeza zimepata ufumbuzi ndani ya ziara hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameushukuru Uongozi wa Jumiya ya Kiislamu ya Al – Fatah chini ya Mkurugeni wake Sheikh Rashid Salim Mohammed kwa jitihada unazochukuwa za kusaidia masuala ya Kijamii katika maeneo mbali mbai hapa Nchini.
Mheshimiwa Hemed alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kufarajika na hatua hiyo yenye kuchangia kustawisha maisha ya Wananchi hasa wale wenye mazingira magumu na kuahidi kwa itatoa msaada katika kuona malengo ya Jumuiya hiyo yanafanikiwa vyema.
Kijiji cha Kibumbwi kilichopakana na Kijiji cha Kiwengwa upande wa Mashariki, Kijiji cha Kipandoni kwa upande wa Kusini na Upenja kwa upande wa Magharibi kina idadi ya Wakaazi Mia 256 wanaojishughulisha na Kilimo na Ufugaji katika harakati zao za Kimaisha kikiwa ndani ya Wadi ya Upenja yenye Idadi ya Wananchi wasiopungua Elfu 2,000.