KIKUNDI cha mazoezi cha Mtu ni Afya Fitness Club cha Kidike, kimesema kinakusidia kutembea shehia hadi shehia, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, ili kuwatayarisha vijana kushiriki katika michezo mbali mbali.
Kauli hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Kojani Hamad Hassan Chande, baada ya kumaliza matembezi yalioanzia Mchangamdogo hadi Madenjani na ufanyaji wa mazoezi ya Viungo, pamoja na kukabidhi Jezi na Fedha taslimu kwa ajili ya bonanza la michezo linalotarajiwa kufanyika Januari Mosi 2021.
Alisema kupitia vikundi hivyo anaamini kwamba upo uwezekano mkubwa wa kuibua vipaji mbali mbali vya michezo, ikiwemo mchezo Riadha, mpira wa miguu na resi za baskeli, ambapo watakua na uwezo wa kushiriki michezo mbali mbali ya kitaifa na kimataifa.
Aliwashajihisha wananchi kuendelea kufanya mazoezi, ili kulinda afya zao, kwani serikali inaelekea kwenye uchumi wa viwanda bila ya kuwa na wananchi wenye afya itakua ni vigumu kuleta mabadiliko ya kiuchumi.
Mbunge huyo aliwataka wananchi kulinda amani na kuiyunga mkono serikali iliyopo madarakani, ili kufanikisha malengo yake kwa wananchi.
“Mazoezi hayachaguwi rika hata watoto wadogo na wazee, vizuri tukashiriki katika mazoezi ikizingatiwa mazoezi ni afya na ajira pekee, wapo wanamichezo wamejariwa kupitia michezo”alisema.
Naye mwanasheria wa kikjundi hicho Shaame farahani Khamis, alisema wapo tayari kushirikiana na mbunge huyo, kwani kikundi chao kinashiriki katika shuhuli mbali mbali za kijamii ikiwemo ufanyaji usafi.
Alisema kikundi chao kinaundwa kutoka shehia mbali mbali, ikiwemo Mjini Ole, Kiuyu, Kangagani, Ole Muhogoni, Ole Kianga, Mbuzini na Uwandani.
“Kikundi chetu ni cha mazoezi hakifungamani na chama chochote wala dini yoyote, sote tumekusanyana hapa kwa lengo la kufanya mazoezi tu”alisema.
Kwa upande wake Dk Hasnuu Faki Hassan aliahidi kutunza amani na kuiyunga mkono serikali iliyopo madarakani ili shuhuli zamichezo zipate kuendelea.
Nao wanamazoezi hao wamesema kuwa yapo mabadiliko makubwa katika afya zao baada ya kushiriki katika mazoezi hayo zaidi ya miaka mitano sasa.
Kikundi hicho kinawafanya mazoezi 80 hadi sasa.